Waziri Mkuu wa Ethiopia atoa wito kwa Afrika kuendeleza Akili Mnemba ya ndani
(last modified Sun, 18 May 2025 09:17:59 GMT )
May 18, 2025 09:17 UTC
  • Waziri Mkuu wa Ethiopia atoa wito kwa Afrika kuendeleza Akili Mnemba ya ndani

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, ametoa wito kwa mataifa ya Afrika kuunganisha nguvu katika kuendeleza teknolojia ya Akili Mnemba (AI) ya ndani, ili kuchochea utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya bara.

Akizungumza katika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Akili Mnemba uliofanyika Jumamosi jijini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, chini ya kaulimbiu “Kutumia Akili Mnemba kwa Mafanikio na Ushirikiano wa Afrika,” Abiy amesisitiza kuwa Afrika inaingia katika enzi mpya ya mageuzi ya kiuchumi na kijamii.

Waziri Mkuu huyo alieleza kuwa Akili Mnemba inayotengenezwa kwa kuzingatia muktadha wa Kiafrika inaweza kuwa kichocheo muhimu cha ustawi jumuishi, kwa kusaidia kufanikisha Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika ambayo ni mkakati wa maendeleo wa miaka 50 wa bara zima.

Abiy ammesema: “Leo tumesimama ukingoni mwa enzi mpya yenye matumaini ya ustawi jumuishi wa bara letu, unaochochewa na ubunifu wa ndani katika Akili Mnemba. Huu ni wakati wa kuharakisha utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika."

Amesitiza umuhimu wa Afrika kuunda  upya Akili Mnemba kwa misingi yake yenyewe, akieleza kuwa Ethiopia inawekeza katika miundombinu ya kidijitali na ukuzaji wa ujuzi wa kiteknolojia kuhusiana na AI, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutafsiri ndoto hiyo kuwa matokeo halisi yanayoonekana.