Sekta zilizoathiriwa zaidi na vita vya Sudan ni umeme na uchukuzi
Sekta za umeme na uchukuzi nchini Sudan zimekuwa miongoni mwa sekta zilizoathiriwa zaidi na mzozo wa miaka miwili kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).
Takwimu rasmi zinasema kuwa, sekta ya umeme imepoteza karibu asilimia 40 ya uwezo wake kutokana na hujuma zilizoenea kwenye maeneo yote ya Sudan. Shirika la Umeme Sudan hivi karibuni lilifichua kwamba ni mitambo miwili tu kati ya 15 ya nchi hiyo inayotumia nishati ya joto ndiyo ambayo infanya kazi hivi sasa na mingine saba imeharibiwa kwa kiasi au kikamilifu, ikiwa ni pamoja na ile iliyoko katika mji mkuu Khartoum.
Abdullah Ahmed Mohamed Ali, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme la Sudan amesema kuwa, zaidi ya transfoma 100,000 zimeharibiwa, wakati karibu asilimia 35 ya uwezo wote na zaidi ya mapipa 20,000 ya mafuta ya transfoma yamepotea. Kukatika umeme kunaendelea katika majimbo kadhaa, huku Jimbo la Kaskazini mwa Sudan likikabiliwa na wimbi la kukatika kabisa umeme tangu mwanzoni mwa mwezi Aprili. Huko mjini Khartoum, mashambulizi ya droni na ndege zisizo na rubani kwenye vituo vya umeme yamesababisha kukatika umeme kwa wingi. Abdul-Qadir Abdoun, mjumbe wa Chama cha Wakulima wa Sudan Kaskazini, amesema kuwa, zaidi ya watu 500,000 wa maeneo hayo wameathiriwa mno na kukatika umeme.
Sekta ya uchukuzi ya Sudan pia imepata hasara kubwa. Wakati maafisa wakiendelea kutathmini kiwango cha uharibifu huo, Waziri wa Uchukuzi wa Suan, Abu Bakr Abu Al-Qasim Abdalla amesema: "Uharibifu mkubwa umeathiri sehemu zote za sekta hiyo, hasa reli, mabehewa, njia za usafiri na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum." Barabara nyingi zinazounganisha maeneo tofauti ya Sudan zimeharibiwa na hivyo kukwamisha shughuli za biashara na usafiri.