Waendesha mashtaka Kenya: Waandamanaji 37 watafunguliwa mashtaka ya ugaidi
Serikali ya Kenya imetangaza kuwa itafungua mashtaka ya ugaidi dhidi ya watu 37 waliokamatwa kwenye maandamano ya kuipinga serikali mwishoni mwa mwezi Juni.
Maandamano ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu yalipofanyika maandamano makubwa ya vijana ya kupinga ongezeko la ushuru katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki, yalishuhudia machafuko makubwa yaliyochanganyika na makabliano kati ya vijana hao na polisi.
Kufuatia maandamano hayo, Polisi ya Kenya ilisema imewakamata watu 485 kwa tuhuma za mauaji, ugaidi na ubakaji, miongoni mwa mashtaka mengine, na kuongeza kwamba kuna watu 37 ambao wangali wanachunguzwa.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Kenya imeeleza katika taarifa kwamba, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameidhinisha na kuwasilisha mashtaka ya ugaidi dhidi ya watu 37 waliofikishwa katika Mahakama ya Sheria ya Kahawa iliyoko viungani mwa mji mkuu Nairobi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, washukiwa hao watazuiliwa hadi Julai 10 wakati mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu rufaa yao dhidi ya mashtaka ya ugaidi.
Hasira kuhusu hali ya uchumi na ulafi wa polisi imezua wimbi la maandamano nchini Kenya tangu Rais William Ruto aingie madarakani mwaka 2022.
Ongezeko la kodi lililokuwa limepangwa kupitishwa na serikali, ambalo lilishutumiwa vikali na vijana wa nchi hiyo, lilisababisha maandamano ya wiki kadhaa mwezi Juni na Julai 2024, ambayo yalikandamizwa vikali na polisi.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yaliishutumu polisi ya Kenya kwa kuhusika na vifo vingi vya waandamanaji pamoja na msururu wa watu waliotoweka huku hatima yao ikiwa haijulikani.../