DRC yaendelea kupambana na mlipuko wa kipindupindu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128186-drc_yaendelea_kupambana_na_mlipuko_wa_kipindupindu
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inaendelea kukabiliana na kuenea kwa kasi kwa ugonjwa wa kipindupindu, ambapo visa vilivyothibitishwa vimefikia 1,601 kote.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Jul 11, 2025 04:12 UTC
  • DRC yaendelea kupambana na mlipuko wa kipindupindu

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inaendelea kukabiliana na kuenea kwa kasi kwa ugonjwa wa kipindupindu, ambapo visa vilivyothibitishwa vimefikia 1,601 kote.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Kinshasa siku ya Alhamisi, Waziri wa Afya ya Umma, Roger Kamba, alisema kuwa taifa linakabiliwa na “janga kubwa la kiafya” kutokana na majanga ya mara kwa mara na wimbi la watu waliokimbia makazi yao. Kipindupindu kimeripotiwa katika mikoa 17 kati ya 26 nchini humo.

Takriban wilaya 137 za afya zimeathirika, huku jimbo la Tshopo likiwa limeathirika zaidi kwa kuripoti visa 793 vya kipindupindu. Waziri pia alieleza kuwa ugonjwa huo unaendelea kuenea sambamba na mzunguko wa ugonjwa wa mpox (homa ya kuambukiza inayofanana na ndui).

Alisema wilaya 11 za afya zinajiandaa kuanza kampeni ya chanjo ya dharura ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

Kamba alisema:"Kwa sasa tunakabiliwa na milipuko miwili ya magonjwa: mpox na kipindupindu. Kuhusu kipindupindu, tupo kwenye wiki ya 27 ya ufuatiliaji wa ugonjwa huu. Kwa kuwa mikoa 17 imeripoti visa vilivyothibitishwa au vinavyoshukiwa, tupo kwenye hatua ya juu ya mlipuko ambao bado unaongezeka.”

Katika mji mkuu wa Kinshasa pekee, visa 130 vikirekodiwa kila wiki.

Kipindupindu ni ugonjwa wa bakteria unaosababishwa na ulaji wa chakula au unywaji wa maji yaliyochafuliwa.

Waziri alieleza kuwa idadi kubwa ya visa vinahudumiwa katika ngazi ya jamii, lakini akawasihi wananchi kuchukua tahadhari kwa kufuata usafi wa mazingira, kunywa maji safi, na kufika vituo vya afya mara tu wanapoonesha dalili kama kuhara au kutapika — badala ya kutumia dawa kiholela majumbani.

Mamlaka ya afya nchini DRC ilitangaza rasmi mlipuko wa kipindupindu mwezi Mei mwaka huu, baada ya maabara kuthibitisha kuwepo kwa visa katika mikoa kadhaa.

Tangu tangazo hilo, takriban visa vinavyoshukiwa kufikia 33,000 vimeripotiwa, huku kiwango cha vifo kitaifa kikifikia asilimia 2, kutokana na changamoto ya kuwafikia wagonjwa kwa haraka na kuwapa matibabu sahihi.

Waziri aliongeza kuwa uhaba wa dawa na vifaa muhimu unazidi kudhoofisha jitihada za kupambana na kipindupindu, na hivyo akatoa wito wa kuongeza uhamasishaji na ufuatiliaji.

Serikali, kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) na wadau wengine, serikali ya DRC imeanzisha mfumo wa usimamizi wa dharura kwa ajili ya kuratibu hatua za kitaifa , kwa lengo la kusitisha maambukizi na kupunguza vifo vinavyotokana na kipindupindu.

Timu za majibu ya haraka tayari zimepelekwa katika maeneo yaliyoathirika ili kusaidia mamlaka za afya za maeneo husika katika kugundua visa, kufanya uchunguzi na kutoa huduma za kitabibu kwa wagonjwa.