Serikali ya Algeria yafuta Hadhi Maalum kwa Ubalozi wa Ufaransa
Algeria imefuta kadi zote za hadhi maalumu zilizokuwa zimetolewa kwa wafanyakazi wa Ubalozi wa Ufaransa katika bandari na viwanja vya ndege vya nchi hiyo ya Afrika Kaskazini, ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi dhidi ya kile ambacho Algiers inasema ni vikwazo vilivyowekwa kwa wanadiplomasia wake nchini Ufaransa.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria imesema kuwa ubalozi wake mjini Paris unakumbwa na “vikwazo vya mara kwa mara” katika usafirishaji na upokeaji wa mizigo ya kidiplomasia.
Wizara hiyo imeongeza kuwa imemuita kaimu balozi wa Ufaransa kuelezea malalamiko dhidi ya kile ilichokiita “ukiukaji wa wazi wa majukumu ya kimataifa” unaofanywa na serikali ya Ufaransa.
Algiers ilieleza kuwa hatua hiyo, “ambayo awali ilikuwa ikihusu tu Ubalozi wa Algeria nchini Ufaransa,” sasa imepanuliwa hadi ofisi za ubalozi mdogo pia licha ya ahadi zilizotolewa awali na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa kuwa wangefanyia tathmini suala hilo.
Mvutano huu mpya unaongeza msururu wa migogoro ya kidiplomasia kati ya Algeria na Ufaransa, ambao katika miezi ya hivi karibuni umechochewa na mizozo ya mara kwa mara. Nchi hizi mbili zimekuwa zikigongana mara kwa mara kuhusu masuala ya kihistoria baada ya ukoloni, sera za uhamiaji, pamoja na uungaji mkono wa Ufaransa kwa msimamo wa Morocco kuhusu eneo la Sahara Magharibi eneo ambalo Algeria imekuwa ikiliunga mkono katika harakati zake za kutafuta uhuru.
Mwezi Mei, Ufaransa ilitangaza kuwa ingewafukuza wanadiplomasia wa Algeria kufuatia uamuzi wa Algeria wa kuwafukuza zaidi ya maafisa wa Ufaransa kumi na wawili, ambao ilidai waliteuliwa na Paris bila kufuata taratibu rasmi. Mapema mwezi Aprili, nchi zote mbili ziliwafukuza wanadiplomasia 12 kila upande, katika mvutano wa kuli[iza kisasi uliochochewa na kukamatwa kwa afisa mmoja wa Algeria nchini Ufaransa, hali iliyosababisha Paris kumrudisha nyumbani balozi wake.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, alisema karibuni kuwa uhusiano kati ya Ufaransa na Algeria kwa sasa umefikia hali ya “kusimama kabisa,” licha ya juhudi za awali za Rais Emmanuel Macron na mwenzake wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, za kutuliza hali hiyo. Wakati wa mazungumzo kwa njia ya simu mwishoni mwa Machi, viongozi hao wawili walikubaliana kuendeleza mazungumzo, na siku chache baadaye Barrot alisafiri hadi Algiers kwa mazungumzo kuhusu kurahisisha usafiri na kuimarisha ushirikiano wa kibalozi, ambao Paris ilielezea kama “wa kiutendaji na wa kujenga.”