Utekaji nyara wa wafanyakazi wa misaada huko Sudan Kusini ni zaidi ya maradufu
Idadi ya wafanyakazi wa misaada waliotekwa nyara nchini Sudan Kusini imeongezeka zaidi ya mara mbili mwaka huu. Takwimu hii imetolewa na maafisa wawili waandamizi wa masuala ya kibinadamu wanaofanya kazi katika makundi ya kimataifa.
Mashirika ya misaada yana wasiwasi usalama wa wafanyakazi wao na kukatizwa kwa shughuli zao za kunusuru maisha ya raia huko Sudan Kusini.
Ripoti zinasema kuwa, baadhi ya waliotekwa nyara wameachiliwa baada ya makundi yenye silaha kupewa fedha za kikomboleo au mlungura lakini mfanyakazi mmoja wa shirika la misaada aliaga dunia mapema mwezi huu akiwa mikononi mwa watekaji nyara.
Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu umeiorodhesha Sudan Kusini kama moja ya maeneo hatari sana kwa wafanyakazi wa huduma za misaada ya kibindamu.
Hata hivyo weledi wa mambo wanasema kuwa kitendo cha watekaji nyara kutaka kupatiwa kiwango kikubwa cha fedha ili kuwaachia mateka ni mwenendo mpya na unaotishia.
"Wasiwasi mkubwa uliopo sasa ni kuwa mwenendo huu unaweza kuwa kadhia kuu inayoikabili nchi," amesema Daniel Akech Mchambuzi wa Sudan Kusini anayefanya kazi katika Shirika la International Crisis Group.
James Unguba, mfanyakazi wa misaada ya kibinadamu wa Sudan Kusini alitekwa nyara mwezi mwaka huu katika kaunti ya Tambura, katika jimbo la Equatoria Magharibi na kuaga dunia mikononi mwa watekaji nyara tarehe 3 mwezi huu wa Septemba.
Sababu ya kifo cha mfanyakazi huyo haijabainishwa hadi sasa. Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini kwa upande wake ameliambia shirika la habari la AP kwamba hana taarifa kuhusu kifo cha Unguba na amekataa kujibu maswali aliyoulizwa.