Sudan Kusini yamshtaki Makamu wa Rais Machar kwa uhaini, mauaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130702-sudan_kusini_yamshtaki_makamu_wa_rais_machar_kwa_uhaini_mauaji
Riek Machar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini amefunguliwa mashitaka ya mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya binadamu.
(last modified 2025-09-22T12:10:58+00:00 )
Sep 12, 2025 06:46 UTC
  • Sudan Kusini yamshtaki Makamu wa Rais Machar kwa uhaini, mauaji

Riek Machar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini amefunguliwa mashitaka ya mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya binadamu.

Mashtaka hayo yanatokana na madai ya kuhusika kwake katika mashambulizi ya wanamgambo dhidi ya vikosi vya serikali mwezi Machi, Waziri wa Sheria amesema hayo jana Alkhamisi.

Serikali ya Sudan Kusini inadai kuwa, Jeshi Jeupe (White Army), kundi la vijana wanaobeba silaha, lilishambulia kambi ya kijeshi huko Nasir, kaskazini mashariki mwa Sudan Kusini, na kuua zaidi ya wanajeshi 250 kwa amri ya Machar.

Wengine saba, akiwemo waziri wa zamani wa mafuta ya petroli, walishtakiwa pamoja na Machar jana Alkhamisi kufuatia uchunguzi kuhusu njama ya uasi inayodaiwa kupangwa nao.

"Uhalifu huu ulibainishwa na ukiukwaji mkubwa wa Mikataba ya Geneva na sheria za kimataifa za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kunajisi maiti, mateso ya raia na mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa kibinadamu," Waziri wa Sheria, Joseph Geng Akech amenukuliwa na AFP akisema hayo.

Wakati huo huo, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amesaini dikrii ya kumsimamisha kazi Machar, baada ya kiongozi huyo kufunguliwa mashitaka ya uhaini na mauaji.

Ikumbukwe kuwa, Machar alikamatwa kwa tuhuma za kujaribu kuchochea uasi mwezi Machi mwaka huu 2015.  Mivutano na hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka kati ya pande mbili za Rais Salva Kiir na Machar na ikashtadi mnamo mwezi Februari mwaka huu wakati kundi liitwalo Jeshi Jeupe ambalo ni tiifu kwa Machar, lilipovamia kambi ya jeshi jimboni la Upper Nile na kushambulia pia helikopta ya Umoja wa Mataifa.