Mabunge ya Kiarabu na Kiafrika yakosoa kimya cha jamii ya kimataifa kwa jinai za utawala wa Kizayuni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130742-mabunge_ya_kiarabu_na_kiafrika_yakosoa_kimya_cha_jamii_ya_kimataifa_kwa_jinai_za_utawala_wa_kizayuni
Mabunge ya Kiarabu na Kiafrika yamekosoa vikali kimya cha jamii ya kimataifa kwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-09-13T03:51:33+00:00 )
Sep 13, 2025 03:51 UTC
  • Mabunge ya Kiarabu na Kiafrika yakosoa kimya cha jamii ya kimataifa kwa jinai za utawala wa Kizayuni

Mabunge ya Kiarabu na Kiafrika yamekosoa vikali kimya cha jamii ya kimataifa kwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Katika kikao cha dharura mjini Cairo, mabunge ya nchi za Kiarabu na Afrika yametoa taarifa ya kukosoa kimya cha jamii ya kimataifa na ukosefu wa mifumo madhubuti ya kuuwajibisha utawala wa Kizayuni na kusisitiza kuwa: Mtazamo huu kivitendo unauhimiza utawala wa Kizayuni kuendelea na jinai zake.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran Press, Bunge la Kiarabu, linaloongozwa na Mohammed bin Ahmed Al-Yamahi, na Bunge la Afrika, linaloongozwa na Zephania Charumbira, lilifanya mkutano wa dharura mjini Cairo siku ya Ijumaa ili kuchunguza matukio ya hivi karibuni katika eneo hilo.

Mwishoni mwa mkutano huo, mabunge hayo mawili yalitoa taarifa ya pamoja na kuelezea mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya Qatar kuwa ni "uchokozi dhidi ya nchi zote za Kiarabu na Kiafrika" na "ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kanuni za kimataifa."

Washiriki wa mkutano huo pia wamelaani vita vinavyoendelea vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza, na kuvitaja kuwa ni mfano wa "mauaji ya halaiki, mauaji ya kikaumuu, na njaa iliyopangwa" ambayo hadi sasa imegharimu maisha ya maelfu ya raia - wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Mabunge ya nchi za Kiarabu na Afrika pia yamezitaka nchi za dunia kulitambua taifa la Palestina katika kikao kijacho cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.