Wakfu wa Mandela walaani shambulio la Israel dhidi ya msafara wa Sumud
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131622-wakfu_wa_mandela_walaani_shambulio_la_israel_dhidi_ya_msafara_wa_sumud
Wakfu wa Nelson Mandela, taasisi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa kwa ajili ya kumbukumbu ya rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, imelaani amelaani vikali shambulio la utawala wa Israel dhidi ya msafara wa kimataifa wa meli nyingi wa Sumud uliokuwa ukielekea Ukanda wa Gaza, na kutaka kuachiwa mara moja kwa wanaharakati waliotekwa nyara na kuzuiliwa na askari wa majini wa Kizayuni.
(last modified 2025-10-05T10:41:33+00:00 )
Oct 05, 2025 10:41 UTC
  • Wakfu wa Mandela walaani shambulio la Israel dhidi ya msafara wa Sumud

Wakfu wa Nelson Mandela, taasisi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa kwa ajili ya kumbukumbu ya rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, imelaani amelaani vikali shambulio la utawala wa Israel dhidi ya msafara wa kimataifa wa meli nyingi wa Sumud uliokuwa ukielekea Ukanda wa Gaza, na kutaka kuachiwa mara moja kwa wanaharakati waliotekwa nyara na kuzuiliwa na askari wa majini wa Kizayuni.

Wakfu wa Nelson Mandela unabainisha kwa wasiwasi mkubwa ripoti kwamba majeshi ya Israel yamekamata boti zilizokuwa zimebeba wanaharakati kutoka nchi nyingi na misaada ya kibinadamu zikielekea Gaza,” shirika hilo limesema.

"Kama shirika lililopewa mamlaka ya kuhamasisha urithi wa Madiba kwa ajili ya kuundwa kwa jamii zenye haki nchini Afrika Kusini na duniani kote, hatuwezi kukaa kimya wakati mipango ya kibinadamu inazuiwa na wakati wale wanaofanya kazi ya kuendeleza utu wa binadamu wanazuiliwa," wakfu huo uliongeza.

Wakati huo huo, Msemaji wa chama mashuhuri cha upinzani nchini Afrika Kusini cha Economic Freedom Fighters (EFF) Sinawo Thambo pia amelaani kitendo hicho cha kijinai cha utawala haramu wa Israel.

"Utekaji nyara wa raia wa Afrika Kusini na jeshi la kigeni hauwezi kuvumiliwa," amesema Thambo na kuongeza kuwa, "Ulimwenguni kote, hasira zinaongezeka ... huku watu wa kawaida wakichoshwa na mapuuza na ukatili wa Israel. Hakuna uchokozi wa kijeshi utakaozuia harakati za kimataifa za ukombozi wa Palestina."

kablaya hapo, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa siku ya Alkhamisi alitaka kuachiliwa mara moja kwa Waafrika Kusini na raia wengine wa kigeni wanaozuiliwa na jeshi la Israel, baada ya wanajeshi wa majini wa utawala huo haramu kushambulia msafara wa kibinadamu uliokuwa unaelekea Gaza.

Amesema kuwa, hatua za Israel zilikiuka uhuru wa nchi ambazo bendera zao zilipeperushwa kwenye meli za msafara wa Sumud na kukiuka amri ya Mahakama ya Kimataifa inayotaka kufikishwa misaada ya kibinadamu bila vikwazo huko Gaza.  Ramaphosa alisema dhamira ya msafara wa Sumud ilikuwa njia moja ya kutangaza "mshikamano," na wala sio makabiliano, na ameonyesha matumaini kwamba Israel itawaachilia huru haraka wanaharakati iliowateka, akiwemo mjukuu wa Nelson Mandela, Mandla Mandela.