WFP yaonya juu ya kuongezeka njaa miongoni mwa wakimbizi nchini Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131852-wfp_yaonya_juu_ya_kuongezeka_njaa_miongoni_mwa_wakimbizi_nchini_ethiopia
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) jana Ijumaa lilionya kwamba wakimbizi nchini Ethiopia wako katika hatari ya kuteseka zaidi kwa njaa huku uhaba mkubwa wa fedha ukisababisha kupunguzwa mgao wa chakula.
(last modified 2025-10-11T05:35:51+00:00 )
Oct 11, 2025 05:35 UTC
  • WFP yaonya juu ya kuongezeka njaa miongoni mwa wakimbizi nchini Ethiopia

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) jana Ijumaa lilionya kwamba wakimbizi nchini Ethiopia wako katika hatari ya kuteseka zaidi kwa njaa huku uhaba mkubwa wa fedha ukisababisha kupunguzwa mgao wa chakula.

WFP imesema katika taarifa yake kwamba mwezi huu wa Oktoba, imelazimika kupunguza mgao kwa wakimbizi 780,000 katika kambi 27 kwenye maeneo yote ya Ethiopia.

Sehemu moja ya taarifa ya WFP imesema: "Hii ina maana kwamba kila mtu sasa atapokea msaada wa chakula sawa na kalori chini ya 1,000 kwa siku. Njaa na viwango vya utapiamlo viko juu sana miongoni mwa wakimbizi wapya."

Taarifa hiyo pia imebaini kuwa katikati ya upungufu mkubwa wa fedha, ni wakimbizi wapya 70,000 tu waliowasili Ethiopia ambao walikimbia vita katika nchi jirani za Sudan na Sudan Kusini ndio watakaoendelea kupokea mgao kamili kwa muda wa miezi sita ijayo.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limetoa mwito wa kutolewa dola milioni 230 za kuliwezesha kuendeleza shughuli zake za kibinadamu kwa muda wa miezi sita ijayo. 

Vilevile WFP imeendelea kutoa onyo kwa kusema kwamba usambazaji wa vyakula maalumu vya lishe vinavyotolewa kwa watoto na akinamama wenye utapiamlo, pia "unapungua kwa kiwango cha hatari, na unatarajiwa kuisha kabisa ifikapo mwezi Disemba mwaka huu."

Aidha taarifa hiyo imesema kuwa, hali hiyo itailazimisha WFP kusitisha msaada kwa watoto milioni 1 wenye utapiamlo na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, isipokuwa tu kama fedha za ziada zitatolewa na duru na mataifa wafadhili yaliyoahidi kuendelea kudhamini mahitaji ya wakimbizi hao.