Gen-Z Morocco wamlazimisha mfalme kufanya mageuzi ya kimsingi
Mfalme Mohammed wa Sita wa Morocco jana Ijumaa alitoa amri ya kufanyika mageuzi ya kimsingi ili kulinda haki za kijamii wakati huu ambapo nchi hiyo imekumbwa na maandamano yanayoongozwa na vijana wanaolalamikia huduma mbovu za kijamii na ukosefu wa usawa.
Akifungua mwaka mpya wa kutunga sheria, mfalme wa Morocco ametaka kusiwe na mizozo wala kutegeana katika utekelezaji wa miradi ya taifa na maendeleo ya jamii.
Ametaja vipaumbele muhimu vya kutiliwa mkazo zaidi hivi sasa kuwa ni pamoja na kukuza mipango ya ndani ya kiuchumi, kuandaa mazingira ya kupatikana ajira kwa vijana na kustawishwa elimu na afya. Pia ametoa mwito wa kuharakishwa utekelezaji wa ratiba za kupunguza ukosefu wa uadilifu wa kikanda na kuboreshwa hali ya maisha katika maeneo ya milimani na pwani.
Maandamano ya nchi nzima yameenea katika kona zote za Morocco tangu mwishoni mwa Septemba. Wimbi hilo la maandamano lilizuka baada ya takriban wanawake wanane kufariki dunia wakati wa kujifungua katika hospitali ya umma kwenye mji wa kusini mwa nchi hiyo wa Agadir.
Waandamanaji, wengi wao wakiwa vijana, wanataka mageuzi katika huduma za afya na elimu, wakiishutumu serikali kuwa imeelekeza rasilimali katika maandalizi ya kuandaa Kombe la Dunia la FIFA 2030 na Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 badala ya kuboresha huduma za kijamii.
Viongozi wa Morocco wanasema kuwa, watu watatu waliuawa katika makabiliano na vikosi vya kulinda usalama tarehe Mosi mwezi huu wa Oktoba na wengine kadhaa walikamatwa.