Umoja wa Mataifa: Watu milioni 25 wanakabiliwa na baa la njaa Sudan
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vimesababisha mamilioni ya watu kuyakimbia makazi yao na karibu milioni 25 kukumbwa na baa kubwa la njaa.
Umoja wa Mataifa umesema kuwa, hali ya Sudan ni mzozo mkubwa kabisa wa njaa na wakimbizi wa ndani ambao haujashuhudiwa ulimwenguni.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa imelaani kuongezeka machafuko na mauaji ya raia wasio na hatia kufuatia ripoti za vifo vya zaidi ya watu 50 huko El Fasher hii ikiwa ni kulingana na vyanzo vya tiba na vingine vya eneo hilo.
Stéphane Dujarric, msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema, wakati ambapo ulimwengu umejikita kwenye matukio mengine muhimu, sitaki tupuuze hali mbaya na ya kutisha ya Sudan na hasa huko El Fasher ambayo kama inavyojulikana ni mji mkuu uliozingirwa wa Darfur Kaskazini."
Mashambulizi ya karibuni ya wanamgambo wa RSF kwenye mji wa El Fasher ni makubwa zaidi tangu kuanza kwa vita nchini humo Aprili, 2023. Mji huo umezingirwa na RSF tangu mwaka uliopita. RSF inafanya mashambulizi ya karibu kila siku kwenye makambi ya watu waliyoyakimbia makazi yao na maeeneo yanayouzunguka mji huo na kuwaua mamia ya raia huku ikizuia njia salama za manusura kuondoka.
Sudan ilitumbulia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Aprili mwaka 2023, kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na Abdel Fattah al-Barhan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) chini ya amri ya Hamdan Dagalo.