Uchaguzi wa Cameroon unafanyika leo huku Biya akitarajiwa kushinda muhula wa nane
Wananchi wa Cameroon waliotimiza masharti ya kupiga kura leo Jumapili (12 Oktoba) wanaelekea katika vituo vya kupigia kura kushiriki katika uchaguzi wa Rais.
Vituo vya kupigia kura vinatarajiwa kufunguliwa mapema asubuhi ya leo, huku Tume ya Uchaguzi ikisema kuwa, maandalizi yote kwa ajili ya uchaguzi huo yamekamilika.
Rais Paul Biya, 92, kiongozi wa nchi mwenye umri mkubwa zaidi duniani, aliingia madarakani mwaka wa 1982.
Akiwa yuko madarakani kwa takribani miaka 43, Paul Biya anawania muhula wa nane wa miaka mingine saba ya kuendelea kubaki madarakani.
Biya mara kwa mara husafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, na mwaka jana uvumi ulienea kwamba alikuwa amefariki dunia, uvumi ambao serikali iliukanusha vikali hadharani.
Nchi hiyo ya Afrika ya Kati inayozalisha kakao na mafuta imekumbwa na changamoto katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kupanda kwa gharama ya chakula, kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira kwa vijana, mashambulizi ya silaha kaskazini mwa nchi na mzozo wa kujitenga katika mikoa ya kusini mwa nchi hiyo inayozungumza Kiingereza.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Cameroon Paul Atanga Nji amewaonya wagombea wanaoshiriki uchaguzi wa rais leo Jumapili dhidi ya kudai ushindi kabla ya matokeo rasmi kutangazwa na baraza la katiba.
"Wale ambao watajaribu kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais au ushindi wowote wa kujitangaza wenyewe kwa kukiuka sheria za jamhuri watakuwa wamevuka mstari mwekundu," alionya.