Wahamiaji wanaorejea Guinea waelezea magumu wanayokabiliana nayo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133052-wahamiaji_wanaorejea_guinea_waelezea_magumu_wanayokabiliana_nayo
Maelfu ya raia wa nchi za Afrika wamerejea katika nchi zao kwa msaada wa mpango wa hiari wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM na kuelezea matatizo makubwa waliyokumbana nayo wakiwa katika ukimbizi.
(last modified 2025-11-11T07:20:19+00:00 )
Nov 11, 2025 07:20 UTC
  • Wahamiaji wanaorejea Guinea waelezea magumu wanayokabiliana nayo

Maelfu ya raia wa nchi za Afrika wamerejea katika nchi zao kwa msaada wa mpango wa hiari wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM na kuelezea matatizo makubwa waliyokumbana nayo wakiwa katika ukimbizi.

Baadhi ya wakimbizi hao waliorejea nchini Guinea baada ya kufeli ndoto zao za kufika barani Ulaya ni huyu aliyejitambulisha kwa jina la Kabinet Kante mwenye umri wa miaka 20. Anasema ndoto yake ilikuwa ni kucheza soka ya kulipwa barani Ulaya. Anaendelea kusema: Baada ya kurejea kwao Guinea anahisi amekombolewa. Alijaribu kufika barani Ulaya, akifanya safari za hatari kupitia Mali na Algeria, kabla ya hatimaye kutumia miaka miwili nchini Tunisia akijaribu kufika huko Ulaya bila ya mafanikio.

Anasema, wakati alipojaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kuelekea barani Ulaya, alikamatwa na maafisa waa Tunisia ambao walimchukua yeye na kundi la wahamiaji na kuwatupa jangwani wakakwama huko bila ya maji wala chakula.

Anaendelea kusimulia kisa chake akisema, mwanamme mmoja raia wa Mali waliyekutana naye barabarani aliwaambia wafuate njia kwenye alama ya matairi ya gari linalopita ndipo wangeweza kurejea Tunisia. Kundi hilo lilitumia wiki mbili barabarani kurejea Tunisia.

Mwezi Julai, akiwa amekata tamaa na hana cha kufanya, Kante alirudishwa Guinea kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa na sasa anasema ameacha ndoto yake ya kucheza soka ya kulipwa, na anataka tu kujipatia riziki ya halali. Changamoto kubwa iliyoko nchini Guinea ni kwamba hakupatikani kazi zenye malipo mazuri, hata kwa wasomi na wenye shahada za juu.

Vile vile Kante anasema afya yake ya akili imeharibika na IOM haijampa msaada iliomuahidi kabla ya kukubali kurejea Guinea kwa hiari.