Zaidi ya asilimia 70 ya Wasudan wanaishi chini ya kiwango cha umaskini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133066-zaidi_ya_asilimia_70_ya_wasudan_wanaishi_chini_ya_kiwango_cha_umaskini
Umaskini nchini Sudan umeongezeka zaidi ya mara tatu tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo Aprili 2023. Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Ustawi wa Jamii, Mutasim Ahmed Saleh.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Nov 11, 2025 23:01 UTC
  • Zaidi ya asilimia 70 ya Wasudan wanaishi chini ya kiwango cha umaskini

Umaskini nchini Sudan umeongezeka zaidi ya mara tatu tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo Aprili 2023. Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Ustawi wa Jamii, Mutasim Ahmed Saleh.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Waziri Saleh amesema kuwa takriban raia milioni 23 wa Sudan kwa sasa wanaishi chini ya mstari wa umaskini.

Amenukuliwa na gazeti la Sudan Tribune akisema: “Kiwango cha umaskini nchini Sudan kimepanda kutoka asilimia 21 hadi asilimia 71 kutokana na vita, kwa mujibu wa ripoti rasmi."

Waziri huyo amehusisha ongezeko hilo kubwa la umaskini na mzozo unaoendelea kati ya Jeshi la Sudan na waasi wa RSF. Amesema serikali inapanga kukabiliana na janga hilo kwa kupanua fursa za ajira na programu za maendeleo zinazolenga kufufua sekta za uzalishaji. Aidha ameahidi kuanzisha mageuzi ya kifedha ili kuwawezesha wazalishaji wa ndani kupata mitaji kwa urahisi.

Mgogoro huo umeharibu uchumi wa ndani na kuwalazimisha mamilioni ya watu kukimbia makazi yao.

Mnamo Oktoba 26, RSF ilidai kuchukua udhibiti wa mji wa Al Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini, pamoja na makao ya Kamandi ya Kikosi cha Sita cha Jeshi la Sudan. Baadaye, Umoja wa Madaktari wa Sudan uliripoti kuwa zaidi ya watu 2,200 waliuawa ndani ya saa chache baada ya waasi kuingia mji huo, huku wengine 390,000 wakifurushwa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Novemba kutoka Shirika la Uainishaji wa Awamu za Usalama wa Chakula (IPC), takriban watu milioni 21.2 ,  sawa na asilimia 45 ya idadi ya watu wa Sudan ,walikuwa wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula mnamo Septemba, hasa katika maeneo ya Al Fasher na Kadugli.

Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imebainika kuwa mfadhili mkuu wa kimataifa wa waasi wa RSF kwa kuwapa msaada wa kijeshi na kifedha unaohitajika kwa kampeni ya mauaji ya kimbari.