UN: Mapigano yanashadidi mashariki mwa DRC
Mapigano yanayoendelea kukithiri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) yamesababisha vifo vya zaidi ya raia 70, kuwafurusha makwao zaidi ya watu 200,000 na kuwakosesha maelfu ya watu msaada wa chakula.
Hali hiyo imepelekea Umoja wa Mataifa kutoa tahadhari Alhamisi kuhusu dharura ya kibinadamu inayoongezeka kwa kasi na kuvuka mipaka.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu wa Masuala ya Kibinadamu na Msaada wa Dharura OCHA, imesema hali katika jimbo la Kivu Kusini imezorota kwa kasi tangu tarehe 2 Desemba kutokana na mapigano mazito katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Uvira, Walungu, Mwenga, Shabunda, Kabare, Fizi na Kalehe.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, wanachama wa kundi la waasi la M23 waliingia katika jiji muhimu la Uvira Jumatano na wakazi wameripoti hali ya hofu na kutojiamini
Kwa mujibu wa Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesitisha shughuli zote katika jimbo la Kivu Kusini, na hivyo kuwakata kwenye msaada wa chakula unaookoa maisha watu 25,000.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa siku chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, kuituhumu Rwanda kwa kukiuka makubaliano ya 'amani' yaliyosimamiwa na Marekani na kutiwa saini wiki iliyopita mjini Washington DC.
Makubaliano hayo, yaliyosimamiwa na Rais Donald Trump, yamekosolewa vikali na wachambuzi wengi wanaosema yamelenga zaidi kurahisisha uhamishaji wa madini adimu kutoka mashariki mwa DRC kuliko kuleta amani ya kweli katika eneo hilo. Trump mwenyewe amesema baada ya mapatano hayo, makampuni ya kiteknolojia ya Marekani yataweza kuchimba madini ya DRC, jambo linaloweka wazi nia yake ya kupora madini ya nchi hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Edouard Bizimana, ametuhumu Rwanda kwa kuendeleza “harakati za kuvuruga usalama” mpakani na DRC. Amesisitiza kuwa majeshi ya Burundi yaliyotumwa mashariki mwa DRC hayataondoka hadi “jukumu lao litakapokamilika kikamilifu.”
Takribani askari 15,000 wa Burundi wameripotiwa kuwa mashariki mwa DRC wakisaidia jeshi la nchi hiyo kupambana na waasi.