Rais Samia apokea hati za utambulisho za balozi wa Iran nchini Tanzania
-
Rais Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan (kulia) akiwa na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Hemmatpanah
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, jana alipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa mabalozi wapya watano walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao, katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma.
Balozi Mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Hemmatpanah alijiunga na mabalozi Angola, Slovakia, Namibia na Uholanzi kukabidhi hati za utambulisho.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Ikulu, Rais Samia aliwakaribisha Mabalozi hao na kusisitiza dhamira ya Tanzania kuendeleza uhusiano wa kirafiki na ushirikiano unaojengwa juu ya kuheshimiana, malengo ya pamoja ya maendeleo na historia ya mahusiano kati ya Tanzania na nchi wanazotoka. Aidha, alibainisha kuwa Tanzania ina nia ya dhati ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji, hususan katika maeneo yenye fursa kama vile kilimo, uongezaji thamani mazao, nishati pamoja na maji.
Rais Samia pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika sekta za afya, elimu, uchumi wa buluu, utalii, teknolojia.
Katika sekta ya elimu, alieleza dhamira ya Serikali ya kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana kupitia ushirikiano na nchi zenye utaalamu wa kiteknolojia ili kuwapatia vijana ujuzi utakaowezesha kuajiriwa au kujiajiri.
Aidha, Rais Samia alizipongeza nchi hizo kwa mchango wao katika safari ya maendeleo ya Tanzania, na kuhimiza ushirikiano wa kina zaidi unaoendana na Dira 2050 na Sera ya Mambo ya Nje inayotilia mkazo diplomasia ya uchumi, ushirikiano wa kimkakati na ushiriki hai katika majukwaa ya kikanda na kimataifa.
Katika hatua nyingine, Rais Samia aliwahakikishia Mabalozi hao hali ya amani, utulivu na usalama nchini, akisisitiza kuwa Tanzania inabaki kuwa mahali salama kwa wananchi wake, wawekezaji na wafanyabiashara.
Alimalizia kwa kuwahakikishia Mabalozi hao ushirikiano kamili kutoka kwa Serikali ya Tanzania wanapoanza majukumu yao, sambamba na matumaini kwamba uwepo wao utazaa fursa mpya za ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili.
Ushirikiano wa Iran na Tanzania unajikita zaidi katika sekta za biashara, nishati, teknolojia, kilimo, afya na elimu.