Upinzani mkubwa wa UN dhidi ya kubadilishwa mipaka ya Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i134228-upinzani_mkubwa_wa_un_dhidi_ya_kubadilishwa_mipaka_ya_gaza
Umoja wa Mataifa umetangaza upinzani wake mkubwa dhidi ya kufanyika mabadiliko ya aina yoyote ya mipaka ya Gaza na utawala wa Israel.
(last modified 2025-12-12T12:25:49+00:00 )
Dec 12, 2025 12:25 UTC
  • Upinzani mkubwa wa UN dhidi ya kubadilishwa mipaka ya Gaza

Umoja wa Mataifa umetangaza upinzani wake mkubwa dhidi ya kufanyika mabadiliko ya aina yoyote ya mipaka ya Gaza na utawala wa Israel.

Baada ya kamanda wa jeshi la Israel huko Gaza kuainisha mpaka mpya, Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba unapinga vikali mabadiliko yoyote ya mpaka wa eneo la Gaza na Israel.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric alisema Jumanne iliyopita kwamba hatua ya Israel ya kutambua "Mstari wa Njano" uliotajwa katika mpango wa kusitisha mapigano wa Rais wa Marekani, Donald Trump kama mpaka mpya inaonekana kuwa "kinyume na muhtawa na matini" ya makubaliano hayo. Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba UN "inapinga vikali mabadiliko yoyote ya mipaka ya Gaza na Israel." Dujarric ameeleza kwamba Umoja wa Mataifa unapozungumzia Gaza, una maana ya mpaka mkuu, "sio mpaka ulio ndani ya mstari wa njano."

Matamshi haya yametolewa baada ya kauli ya Eyal Zamir, Mkuu wa Majeshi ya Israel, ambaye alisema kwamba "Mstari wa Njano sasa ndio mpaka mpya wa Gaza." Zamir pia amesema kwamba Israel itadumisha "udhibiti wa sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza." Utawala wa Israel bado unakalia kwa mabavu zaidi ya asilimia 50 ya Ukanda wa Gaza chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano, na Mstari wa Njano unatenganisha vituo vya kijeshi vya utawala huo na maeneo ambayo Wapalestina wanaruhusiwa kuingia. 

Makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza yalianza kutumika Oktoba 10 kwa mujibu wa mpango wa Donald Trump wenye vifungu 20 na kusimamisha kwa kiasi fulani mashambulio ya miaka miwili ya Israel ambayo yameua zaidi ya Wapalestina 70,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuwajeruhi wengine karibu 171,000 tangu Oktoba 2023. Hata hivyo, Israel inaendelea kukiuka makubaliano hayo kwa kutumia visingizio mbalimbali.

Tangazo la Umoja wa Mataifa la kupinga mabadiliko yoyote katika mipaka ya Ukanda wa Gaza na utawala wa Kizayuni si tu jibu la kisiasa, bali pia linatokana na kanuni za sheria za kimataifa na wajibu wa shirika hilo wa kudumisha amani na usalama duniani. Mojawapo ya sababu kuu za upinzani wa Umoja wa Mataifa ni kufuata kanuni ya kutobadilisha mipaka kwa nguvu. Mkataba wa Umoja wa Mataifa unatangaza waziwazi uvamizi wowote au mabadiliko ya mipaka kwa kutumia nguvu za kijeshi kuwa ni kinyume cha sheria. Hatua ya Israel ya kuanzisha Mstari wa Njano kama mpaka mpya, kwa kweli ni jaribio la kulazimisha hali iliyopo sasa uwanjani kwa jamii ya kimataifa, jambo ambalo Umoja wa Mataifa unaliona kama ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Shirika hilo linasisitiza kwamba mipaka ya Gaza ni ileile iliyotambuliwa hapo awali na kwamba hakuna mabadiliko ya upande mmoja yanayoweza kuchukua nafasi yake.

Sababu nyingine ya upinzani wa Umoja wa Mataifa ni matokeo mabaya kibinadamu na kijamii ya mabadiliko hayo. Utawala wa Israel umesababisha mgogoro mkubwa wa binadamu kwa kuweka vikwazo vikali vya kuingizwa bidhaa na vifaa muhimu eneo la Gaza. Ripoti zinaonyesha kuwa ni sehemu ndogo tu ya malori yaliyobeba chakula, dawa na mafuta yaliyoruhusiwa kuingia Gaza, jambo ambalo limesababisha uhaba mkubwa wa rasilimali muhimu na kuzidisha mateso ya watu. Kubadilishwa mipaka ya Gaza kutakuwa na maana ya kuimarisha vikwazo hivyo na kuwanyima watu wa Gaza haki zao za msingi. Umoja wa Mataifa, kwa kuzingatia wajibu wake wa kibinadamu, haupaswi kukubali hali kama hiyo.

Katika mtazamo wa kisiasa, Umoja wa Mataifa unaamini kwamba kubadilisha mipaka kutadhoofisha sana mchakato wa amani. Mikataba ya kusitisha mapigano na mipango ya amani ya kimataifa inategemea mipaka iliyowazi na inayotambulika. Hatua yoyote ya upande mmoja ya kubadilisha mipaka itabatilisha makubaliano hayo, kuharibu hali ya kuaminiana kati ya pande mbili na kufungua duru mpya ya vurugu na mapigano. Umoja wa Mataifa unasisitiza kwamba suluhisho pekee endelevu la mgogoro wa Gaza ni mazungumzo na makubaliano ya pande zote mbili, si kutwisha masharti na upande mmoja.

Wanajeshi vamizi wa Israel, Ukanda wa Gaza

Umoja wa Mataifa pia una wasiwasi kwamba kubadilisha mipaka kunaweza kuwa mtindo hatari katika mahusiano ya kimataifa. Ikiwa jamii ya kimataifa itaruhusu utawala wa Kizayuni kubadilisha mipaka yake kwa kutumia nguvu za kijeshi, jambo hili linaweza kuwa sababu ya kurudiwa vitendo hivyo katika sehemu zingine za dunia na kutishia vibaya nidhamu ya kimataifa. Hivyo basi, upinzani mkubwa wa Umoja wa Mataifa dhidi ya jambo hilo, kwa hakika, ni ujumbe wa wazi kwa serikali zote kwamba kubadilisha mipaka kunawezekana tu kupitia makubaliano ya kisheria na halali.