Mamia ya askari wa Afrika Magharibi wanaendelea 'kusafisha' Benin
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134236-mamia_ya_askari_wa_afrika_magharibi_wanaendelea_'kusafisha'_benin
Waziri wa Mambo ya Nje wa Benin amesema wanajeshi wapatao 200 wa Afrika Magharibi, wengi wao kutoka Nigeria na Ivory Coast, wako nchini Benin kuiunga mkono serikali kufuatia mapinduzi yaliyofeli Jumapili iliyopita.
(last modified 2025-12-13T02:33:14+00:00 )
Dec 13, 2025 02:33 UTC
  • Mamia ya askari wa Afrika Magharibi wanaendelea 'kusafisha' Benin

Waziri wa Mambo ya Nje wa Benin amesema wanajeshi wapatao 200 wa Afrika Magharibi, wengi wao kutoka Nigeria na Ivory Coast, wako nchini Benin kuiunga mkono serikali kufuatia mapinduzi yaliyofeli Jumapili iliyopita.

Hii ni mara ya kwanza kwa maafisa wa Benin kutangaza hadharani idadi ya wanajeshi wa kigeni waliotumwa nchini humo, ingawaje haijulikani wazi ikiwa baadhi ya askari hao wameshaondolewa nchini humo tangu Jumapili au la.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Benin, Olushegun Adjadi Bakari amesema baadhi ya wanajeshi wa kikanda waliotumwa kusaidia wamebaki nchini "kama sehemu ya operesheni ya kufagia na kusafisha".

Mapema Jumapili, kundi la wanajeshi waliojitambulisha kama “Kamati ya Kijeshi ya Ujenzi Mpya” (CMR) lilitwaa televisheni ya taifa na kutangaza kuwa “Bwana Patrice Talon ameondolewa madarakani kama rais wa jamhuri.”

Tangazo hilo lilijibiwa haraka na mashambulizi ya kutoka kwa vikosi vya askari watiifu kwa Talon.  Jaribio hilo lilisambaratishwa kabisa kufuatia mashambulizi ya anga kutoka Nigeria na kupelekwa kwa wanajeshi kutoka mataifa mengine ya ukanda huo.

Vyanzo vya kijeshi na usalama vya Benin vilisema wanajeshi kadhaa, wakiwemo waliopanga jaribio hilo lililofeli wamekamatwa.

Ukanda wa Afrika Magharibi umekumbwa na wimbi la mapinduzi katika miaka ya karibuni, ikiwemo majirani wa kaskazini mwa Benin, Niger na Burkina Faso pamoja na Mali, Guinea na hivi karibuni Guinea-Bissau.