DRC: Watu 1,500 wameuawa mashariki mwa nchi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135010-drc_watu_1_500_wameuawa_mashariki_mwa_nchi
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema zaidi ya raia 1,500 wameuawa katika ghasia zinazoendelea katika jimbo la Kivu Kusini, mashariki mwa nchi hiyo tangu mapema mwezi Desemba, 2025 mpaka sasa.
(last modified 2026-01-14T11:42:18+00:00 )
Jan 02, 2026 02:47 UTC
  • DRC: Watu 1,500 wameuawa mashariki mwa nchi

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema zaidi ya raia 1,500 wameuawa katika ghasia zinazoendelea katika jimbo la Kivu Kusini, mashariki mwa nchi hiyo tangu mapema mwezi Desemba, 2025 mpaka sasa.

Katika taarifa, serikali ya DRC imesema mapigano yameshtadi katika maeneo kadhaa ya jimbo hilo, haswa kando ya maeneo ya Kamanyola-Uvira, ambapo operesheni za silaha zimesababisha watu wengi kuhama makazi yao.

Wakati huo huo, zaidi ya watu 500,000 wamelazimika kukimbia makazi yao huku kukiwa na ukosefu wa usalama, limeripoti shirika la habari la Xinhua.

Serikali ya DRC imesema kuwa, hatua kwa hatua, medani ya vita imehamia kusini, na kuathiri maeneo mengi ya Kivu Kusini, ikiwa ni pamoja na Uvira, Fizi na Mwenga.

Mamlaka za DRC zinalihusisha ongezeko hilo na makundi yenye silaha yanayoendeleza harakati zao katika eneo hilo, na kuyashutumu kwa kukiuka makubaliano yaliyopo na sheria za kimataifa za kibinadamu.

Kadhalika serikali ya Kinasha imesisitiza azma yake ya kurejesha utawala wa serikali nchi nzima na kuwawajibisha waliohusika na ghasia na mapigano kupitia njia za kidiplomasia na mahakama.

Eneo la mashariki mwa DRC limekumbwa na miongo kadhaa ya ukosefu wa utulivu, hali ambayo imekuwa mbaya zaidi tangu kuibuka tena kwa kundi la waasi la M23 mwishoni mwa 2021.

Serikali ya Kinshasa imekuwa ikiishutumu mara kwa mara nchi jirani ya Rwanda kwa kuunga mkono kundi hilo, madai ambayo serikali ya Kigali imeyakanusha vikali.