Rwanda yakiri kushirikiana na waasi wa AFC/M23
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135940-rwanda_yakiri_kushirikiana_na_waasi_wa_afc_m23
Rwanda imekiri kwa mara ya kwanza kwamba, inashirikiana na kundi la waasi wa AFC/M23 katika harakati za kiusalama huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
(last modified 2026-01-26T23:04:55+00:00 )
Jan 26, 2026 23:04 UTC
  • Rwanda yakiri kushirikiana na waasi wa AFC/M23

Rwanda imekiri kwa mara ya kwanza kwamba, inashirikiana na kundi la waasi wa AFC/M23 katika harakati za kiusalama huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Balozi wa Rwanda nchini Marekani Mathilde Mukantabana ameiambia kamati ya Bunge la Marekani kwamba Rwanda imekuwa ikifanya hivyo kwa sababu za kiusalama lakini pia kuzuia kundi la wapiganaji wa kihutu la FDLR kuendesha mauaji ya jamii ya watutsi wa Kongo.

Hatua ya Rwanda kukiri uhusiano huu na kundi ambalo kwa muda mrefu imekuwa ikikanusha kuliunga mkono imezua mijadala na hisia mseto kuhusu hatua hiyo ya Rwanda.

Katika tangazo lililotolewa na ubalozi wa Rwanda mjini Washington baada ya kikao cha balozi wa Rwanda nchini Marekani Mathilde Mukantabana na kamati ya Bunge la Marekani, Rwanda imekiri kuwa na ushirikiano na AFC/M23 katika utaratibu wa shughuli za kiusalama katika kuwalinda raia wa Kongo wenye asili ya Rwanda hasa wale kutoka kabila la Watutsi ambao tangazo hilo linasema wanaendelea kufanyiwa vitendo vya mauaji na unyanyasaji wa aina nyingine na makundi yenye silaha katika mzozo wa Mashariki ya Congo hasa kundi la wanamgambo wa kihutu la FDLR ambalo Rwanda inasema lilihusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Balozi wa Rwanda nchini Marekani amesema: "Ingawa Rwanda na AFC/M23 wanashiriki katika lengo la pamoja la kuwalinda Watutsi katika DRC dhidi ya wapiganaji wa FDLR na wanamgambo wengine wenye misimamo mikali wanaoungwa mkono najeshi la Kongo FARDC, maslahi ya nchi yangu yanakwenda mbali zaidi ya hilo: kuzuia kujirudia kwa uasi na mauaji ya kimbari yanayovuka mipaka, kama yale ya mwishoni mwa miaka ya 1990, ambayo yanaweza kutishia uwepo wa Rwanda yenyewe”.