Jeshi la Sudan lapata mafanikio katika vita dhidi ya waasi wa RSF
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136226-jeshi_la_sudan_lapata_mafanikio_katika_vita_dhidi_ya_waasi_wa_rsf
Jeshi la Sudan limevunja mzingiro uliowekwa na waasi dhidi ya mji muhimu wa Kusini, Kadugli, Jumanne. Hayo yametangazwa na Rais wa mpito na Mkuu wa Jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.
(last modified 2026-02-04T03:10:15+00:00 )
Feb 04, 2026 03:10 UTC
  • Abdel Fattah al-Burhan
    Abdel Fattah al-Burhan

Jeshi la Sudan limevunja mzingiro uliowekwa na waasi dhidi ya mji muhimu wa Kusini, Kadugli, Jumanne. Hayo yametangazwa na Rais wa mpito na Mkuu wa Jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.

Mji mkuu wa jimbo la Kordofan Kusini, Kadugli, ambapo Umoja wa Mataifa ulisema ulikumbwa na baa la njaa mwaka uliopita, umekuwa chini ya mzingiro kwa sehemu kubwa ya vita vya Sudan vilivyoanza takriban miaka mitatu iliyopita kati ya jeshi na waasi wa RSF.

Al Burhan amesema katika mahojiano mafupi yaliyotangazwa na televisheni ya serikali:
“Hongera kwa wananchi wa Kadugli kwa kuwasili Jeshi la Taifa.”

Ameongeza kuwa, “Jeshi litafika kila sehemu ya Sudan.”

Chanzo cha RSF kilithibitisha kuwa jeshi limechukua udhibiti wa mji huo.

Televisheni ya serikali, Sudan TV, ilionyesha picha za watu Kadugli wakisherehekea na kuonyesha ishara za ushindi wakati maafisa wa jeshi wakiingi katika mji huo.

Mzingiro dhidi ya mji huo uliwekwa na wapiganaji wa RSF na washirika wao, kundi la Sudan People’s Liberation Movement-North linaloongozwa na Abdelaziz al-Hilu.

Kadiri njaa ilivyozidi kuenea, karibu asilimia 80 ya wakazi wa Kadugli, takriban watu 147,000, walilazimika kuondoka katika mji huo.

Eneo pana la Kordofan kwa sasa ndilo eneo lenye mapigano makali zaidi, ambapo mamia ya maelfu wanakabiliwa na njaa.

Baada ya kuteka ngome ya mwisho ya jeshi katika mji wa El-Fasher jimboni Darfur, mwezi Oktoba, RSF ilisonga zaidi ndani ya Kordofan kwa lengo la kudhibiti tena njia kuu ya kati ya Sudan.

Tangu waasi wa RSF waanzishe vita dhidi ya serikali ya Sudan mwezi Aprili 2023, maelfu ya watu wameuawa na wengine  zaidi ya milioni 12 wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi, huku mikoa kadhaa ikikumbwa na njaa na uhaba wa chakula.

Rais Burhan amesisitiza kuwa “hakutakuwa na usitishaji vita maadamu waasi wa  RSF wnaendelea kushikilia miji.”

Serikali ya Sudan inituhumu serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa inawaunga mkono waasi hao wa RSF, tuhuma ambazo nchi hiyo ya Kiarabu imekanusha.