Mkutano wa Tanzania wasisitiza kutumia mashine katika kilimo barani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136264-mkutano_wa_tanzania_wasisitiza_kutumia_mashine_katika_kilimo_barani_afrika
Harakati za zama za sasa za kutumia mashine kwenye sekta ya kilimo barani Afrika lazima zitofautiane na harakati za zamani ili hatua hizo ziwe endelevu. Hayo yamesemwa na Beth Bechdol, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO.
(last modified 2026-02-05T02:34:27+00:00 )
Feb 05, 2026 02:34 UTC
  • Mkutano wa Tanzania wasisitiza kutumia mashine katika kilimo barani Afrika

Harakati za zama za sasa za kutumia mashine kwenye sekta ya kilimo barani Afrika lazima zitofautiane na harakati za zamani ili hatua hizo ziwe endelevu. Hayo yamesemwa na Beth Bechdol, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO.

Hayo yamesemwa na Beth Bechdol, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, akiwa  jijini Dar es salaam nchini Tanzania wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Afrika kuhusu utumiaji endelevu wa mashine kwenye sekta ya kilimo. 

Ufunguzi huo umeanda sanjari na uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Utumiaji wa mashine kwenye kilimo nchini Tanzania mwaka 2026-2036.

 Bi. Bechdol amesema:“Kuleta mashine kubwa bila ufadhili, mafunzo, huduma za matengenezo au kulingana na mazingira ya ndani hakujaleta matokeo ya kudumu. Afrika haihitaji tena vifaa vinavyokaa bila kutumika. Inahitaji mifumo inayofanya kazi,” amesema

Ameongeza kuwa, kwa mtazamo wa FAO, uwepo endelevu wa mashine za kisasa kwenye sekta ya kilimo  ni kichocheo cha mageuzi—sio mashine kuchukua nafasi ya watu, bali zana zinazowawezesha watu, kupunguza kazi nzito na kuwapa wanawake nafasi ya kulima kwa tija zaidi.

Ili kufanikisha mabadiliko haya, amesema, kunahitajika suluhu zinazoongozwa na ushahidi, uzalishaji na mifumo ya huduma ya ndani iliyo imara, mifumo bunifu ya ufadhili, sera wezeshi, na—zaidi ya yote—ushirikiano.

Akifungua mkutano huo,  Waziri Mkuu wa Tanzania Mwigulu Nchemba amesema matumizi ya mashine kwenye sekta ya kilimo ni hitaji la kimkakati: “kupitia vitendo, tunaweza kubadilisha kilimo cha Afrika kiwe sekta iliyo na matumizi endelevu ya mashine kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.”

Mkutano huo ambao unaendelea  hadi tarehe Februari 6 umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya FAO, serikali ya Tanzania na unakutanisha wawakilishi wa serikali, sekta binafsi, watafiti, washirika wa maendeleo, vijana na wakulima ili kubadilishana uzoefu, kujenga ushirikiano na kubaini suluhu zinazoweza kupanuliwa kwa ajili ya kuendeleza matumizi endelevu ya mashine kwenye sekta ya kilimo barani Afrika..