Kesi ya kupinga ushindi wa Museveni yatupiliwa mbali, sababu.. gharama kubwa
-
Rais Yoweri Museveni
Kesi iliyowasilishwa mahakamani kupinga ushindi wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda katika uchaguzi mkuu wa Januari 15 imetupiliwa mbali.
Kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa na mgombea urais, Robert Kasibante wa chama cha NPP katika Mahakama ya Juu baada ya Museveni kutangazwa mshindi.
Katika notisi ambayo iliwasilishwa mahakamani, Kasibante aliomba kuondoa kesi hiyo pamoja na nyingine aliyowasilisha kukagua fomu zote za uchaguzi, mitambo iliyotumiwa kuwatambua wapigakura na vyombo vingine vilivyotumika katika uchaguzi huo.
Hoja kuu ya Kasibante ni kwamba hataweza kulipa gharama ya ukaguzi na mahitaji ya kiufundi yatakayotumika.
“Kesi hii itahusisha utayarishaji wa data au takwimu nyingi na gharama ambayo itatumika ni ya juu mno,” amesema Kasibante kwenye ombi lake.
Alikiri kuwa kuchanganua data hiyo kutahitaji watalaamu huru kushirikishwa na pesa nyingi zitatumika kufanikisha hilo.
Kuondolewa kesi hiyo mahakamani kumetokea siku chache baada ya Majaji wa Mahakama ya Juu wakiongozwa na Jaji Mkuu Flavian Zeija kuandaa kikao na kubaini hoja nne kuu za kuangaziwa katika kesi hiyo.
Mahakama ya Juu bado haijatenga tarehe ya kusikizwa kwa ombi hilo jipya la Kasibante.
Iwapo mahakama itakubali ombi hilo, basi mipango ya kuapishwa Rais Yoweri Museveni ambaye ameongoza Uganda tangu 1986, itaendelea kama ilivyopangwa.
Tume ya Uchaguzi nchini Uganda ilimtangaza Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais, akiwa na jumla ya kura 7,946,772 ambayo ni asilimia 71.65% ya kura zote zilozopigwa.