Kenya yaanza kuondoa askari Haiti huku kikosi kipya cha UN kikichukua hatamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136412-kenya_yaanza_kuondoa_askari_haiti_huku_kikosi_kipya_cha_un_kikichukua_hatamu
Kenya itapunguza idadi ya maafisa wake wa polisi waliotumwa nchini Haiti baada ya kukamilisha jukumu lao kuu la kuleta uthabiti wa kiusalama. Hayo ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni, Korir Sing’Oei.
(last modified 2026-02-09T02:58:26+00:00 )
Feb 09, 2026 02:58 UTC
  • Wanajeshi wa Kenya nchini Haiti
    Wanajeshi wa Kenya nchini Haiti

Kenya itapunguza idadi ya maafisa wake wa polisi waliotumwa nchini Haiti baada ya kukamilisha jukumu lao kuu la kuleta uthabiti wa kiusalama. Hayo ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni, Korir Sing’Oei.

Ujumbe wa Usalama wa Kimataifa unaoongozwa na Kenya (MSS), ambao tangu Oktoba 2023 umetuma maafisa 735 kama uti wa mgongo wa kikosi chenye jumla ya takriban askari 1,000, utasitisha shughuli zake na nafasi yake kuchukuliwa na Kikosi cha Kukandamiza Magenge (GSF) kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Akizungumza na vyombo vya habari vya ndani, Sing’Oei amesema maafisa wa polisi wa Kenya wamefanikiw kuimarisha uwezo wa Kikosi cha Polisi cha Haiti, kulilinda maeneo nyeti, na kusaidia kuweka msingi wa mfumo endelevu wa usalama wa kimataifa.

Kikosi kipya cha GSF, kilichoidhinishwa chini ya azimio thabiti zaidi la Umoja wa Mataifa, kimeundwa kuendesha operesheni za moja kwa moja dhidi ya magenge ya kihalifu, kikiwa na mpango wa kuwa na zaidi ya wanachama 5,500—wakiwemo pia maafisa kutoka Kenya, Jamaica, Guatemela, Kanada, Bahamas na El Salvador.

Maafisa wa Kenya walioko Haiti wanatoka katika vitengo vya Huduma ya Polisi ya Kenya kama vile Kikosi cha Kukabiliana na Fujo (GSU), Kitengo cha Kupambana na Wizi wa Mifugo, Kitengo cha Kukabiliana na Dharura, na pia kikosi maalum cha Wanawake cha Silaha na Mbinu za Kivita (SWAT Team).

Mwaka uliopita Rais William Ruto alisisitiza kuwa licha ya changamoto maafisa wa Kenya waliweza kudhibiti uwanja wa ndege wa Port-au-Prince, kurejesha ikulu ya rais mikononi mwa serikali, na kufungua barabara muhimu kadhaa.

Ujasiri wa Kenya kujitolea katika mzozo ambao mataifa mengi ya Magharibi yaliepuka umetajwa na wachambuzi kama “mabadiliko ya mkondo wa kidiplomasia.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, alisifu uamuzi huo akisema kuwa “kikosi hicho ni mfano halisi wa mshikamano wa kimataifa kwa vitendo.”