Ethiopia yaitaka Eritrea iondoe haraka vikosi kwenye ardhi yake
-
Ethiopia yaitaka Eritrea iondoe haraka vikosi kwenye ardhi yake
Serikali ya Ethiopia imeitaka nchi jirani ya Eritrea kuondoa haraka wanajeshi wake ambao inadai wako ndani ya eneo lake.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia Gedion Timothewos kupitia barua yake ya amemuambia mwenzake wa Erithrea kuwa, matukio ya siku kadhaa zilizopita yanaashiria kuwa serikali ya Asmara imechagua njia inayochochea mvutano. Barua hiyo imetaka ushirikiano wowote kati ya Eritrea na waasi usitishwe haraka.
Ethiopia imeishurumua Eritrea kwa "uchokozi" ikisema ilikuwa ikifanya ujanja pamoja na waasi wa Ethiopia kaskazini na kuwapa silaha.
Eritrea bado haijatoa maoni kuhusu shutuma hizo lakini hapo awali ilikana wanajeshi wake kuvuka mpaka wa pamoja wa nchi hizo mbili.
Kwa muda mrefu kumekuwa na historia ya mvutano kati ya Ethiopia na Eritrea, ambayo ilijitenga na jirani yake mkubwa miongo mitatu iliyopita, na kuna hofu ya mgogoro mpya.
Nchi hizo zilipigana vita vya mpaka kati ya 1998-2000 ambapo zaidi ya watu 100,000 waliuawa.
Mkataba wa amani haukutekelezwa kikamilifu na uhusiano ulipungua tu baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, ambaye baadaye alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel kwa juhudi zake, kusafiri hadi mji mkuu wa Eritrea, Asmara, mwaka wa 2018.
Nchi hizo mbili zilikuwa washirika katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya hivi karibuni vya Ethiopia wakati Eritrea ilipounga mkono jeshi lake dhidi ya vikosi vya wanamgambo wa jimbo la Tigray, lakini mambo yameharibika tena.
Mahusiano yalizorota baada ya Ethiopia kusaini makubaliano ya amani ambayo hayakuihusisha Eritrea mwaka 2022. Mvutano waa sasa unatishia mustakabali wa uhusiano baina ya mataifa hayo mawili jirani.