Jeshi la Libya: Tumekomboa msikiti na jela Sirte kutoka mikononi mwa Daesh
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13768-jeshi_la_libya_tumekomboa_msikiti_na_jela_sirte_kutoka_mikononi_mwa_daesh
Vikosi vya jeshi Libya vimetangaza kuwa vimeukomboa msikiti mkuu wa mji wa Sirte na jela ya mji huo kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, katika operesheni ya kulitimua kundi hilo la kigaidi katika mji huo ulioko kwenye pwani ya kusini ya Ghuba ya Sidra.
(last modified 2026-04-29T03:42:39+00:00 )
Aug 22, 2016 11:35 UTC
  • Jeshi la Libya: Tumekomboa msikiti na jela Sirte kutoka mikononi mwa Daesh

Vikosi vya jeshi Libya vimetangaza kuwa vimeukomboa msikiti mkuu wa mji wa Sirte na jela ya mji huo kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, katika operesheni ya kulitimua kundi hilo la kigaidi katika mji huo ulioko kwenye pwani ya kusini ya Ghuba ya Sidra.

Vikosi hivyo ambavyo askari wake wengi ni brigedi za mji wa Misrata vimeeleza kuwa vinakaribia kuukomboa mji mzima wa Sirte baada ya kukomboa sehemu kubwa ya mji huo katika operesheni inayoendelea kwa mwezi wa tatu sasa.

Kwa mujibu wa msemaji wa hospitali ya Misrata, Akram Gliwan, wapiganaji wasiopungua tisa wa brigedi hizo waliuawa na wengine 85 walijeruhiwa katika mapigano ya jana Jumapili mjini Sirte.

Vikosi vya Libya vikisonga mbele katika mji wa Sirte

Msemaji wa vikosi vya serikali, Rida Issa amesema wapiganaji wao waliokuwa wakisindikizwa na zana nzito na vifaru walisonga mbele katika viunga vya Bufaraa na kulikomboa jengo moja lililokuwa likitumiwa kama jela na magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh.

Hatimaye vikosi hivyo viliukomboa msikiti mkuu wa Sirte wa Ribat, ambao makamanda waandamizi wa Daesh akiwemo kiongozi wa kiidiolojia wa kundi hilo Turki Ben Ali walikuwa wakiutumia kutolea mihadhara. 

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh lilipouvamia mji wa Sirte

Makumi ya maiti za wapiganaji wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh zimepatikana zimetapakaa katika maeneo mapya yaliyokombolewa katika mji wa Sirte.../