Shoukry: Kuuliwa watoto wa Kipalestina hakuwezi kutajwa kuwa ni ugaidi
(last modified Mon, 22 Aug 2016 16:12:19 GMT )
Aug 22, 2016 16:12 UTC
  • Shoukry: Kuuliwa watoto wa Kipalestina  hakuwezi kutajwa kuwa ni ugaidi

Sameh Shoukry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ameamsha hasira katika Ulimwengu wa Kiarabu Jumapili hii baada ya kusema kuwa vitendo vinavyofanywa na Israel haviwezi kutajwa kuwa ni ugaidi dhidi ya raia wa Palestina.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ameyasema hayo katika kikao cha wanafunzi kilichofanyika jana katika Wizara ya Mambo ya Nje huko Cairo likiwa ni jibu alilolitoa baada ya kuulizwa swali na wanafunzi kwamba, kwa nini serikali ya Misri hailaani na kuzitaja hatua zinazochukuliwa na Israel na Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati yakiwemo mauaji ya watoto wa Palestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni kuwa ni za kigaidi. Sameh Shoukr aliendelea kujibu kuwa, hakuna chochote cha kudhania kuwa, upo uhusiano kati ya Israel na makundi ya kigaidi.

Watoto wa Kipalestina waliouliwa katika mashambulizi ya Israel Ukanda wa Ghaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri aliendelea kutetea hatua alizozitaja kuwa ni za kujihami za Israel kwa kusema, nguvu iliyonayo Israel katika uwanja wa kiulinzi ni matokeo ya changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikitishia usalama wa utawala huo tangu kuasisiwa kwake mwaka 1948. Kufuatia matamshi hayo, baadhi ya duru za habari za Kiarabu zimemkosoa na kumshambulia kwa maneno yake hayo ya kuitetea Israel ambapo gazeti moja la Kiarabu lenye makao yake mjini London limeandika makala chini ya kichwa cha maneno kisemacho" Samih Shoukr: Mauaji ya Watoto wa Kipalestina yanayofanywa na Israel si ugaidi." Itakumbukwa kuwa miezi kadhaa iliyopita Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Misri aliitembelea Israel ambapo alikuwa na mazungumzo ya kina na Waziri Mkuu wa utawala huo Benjamin Netanyahu, ziara ambayo ilikuwa ya siri na kutojulikana hadi dakika ya mwisho. 

Sameh Shoukry na Benjamin Netanyahu mjini Tel Aviv miezi kadhaa hivi karibuni