Serikali ya Libya yapigiwa kura ya kutokuwa na imani nayo
Serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imepata pigo kubwa baada ya wabunge katika bunge la nchi hiyo linalotambuliwa kimataifa kuikataa.
Msemaji wa bunge la Libya amesema kuwa wabunge 101 jana walihudhuria bungeni; idadi ambayo inatosha kukidhi kiwango kinachohitajika katika kupiga kura. Abdullah Ablahig ameongeza kuwa wabunge 61 walipiga kura ya kuipinga serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya, 39 hawakupiga kura na mbunge mmoja alipiga kura ya kuiunga mkono serikali hiyo. Nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ilikuwa imegawanyika kati ya serikali na mabunge pinzani. Mbunge wa Libya Abdusalam Nassiya amesema kuwa serikali inapasa kufanyiwa mabadiliko hivi sasa na kuwajumuisha watu zaidi kutoka Tobruk, mji ambao ndio makao makuu ya bunge. Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya ilipatikana kufuatia juhudi za miezi kadhaa za Umoja wa Mataifa za kuzipatanisha pande hasimu zinazozozana nchini humo. Pande mbili hizo yaani serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa yenye makao yake Tobruk mashariki mwa nchi, na ile inayoungwa mkono na wanamgambo yenye makao yake huko Tripoli magharibi mwa nchi, zilifikia mapatano mwaka jana kwa minajili ya kuasisi serikali ya umoja wa kitaifa.
Fayez Serraj aliyeteuliwa mwezi Disemba mwak jana na Umoja wa Mataifa kuongoza serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya, alikuwa akisubiri kura hiyo ya imani ya bunge lenye makao yake huko Tobruk.