Wanawake wako katika hatari kubwa ya kuathiriwa na mlipuko wa Ebola Kongo
-
Wanawake wako katika hatari kubwa ya maambukizi ya Ebola Kongo
Wakati Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiendelea na mapambano dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola, wanawake nchini humo wametajwa kuwa kundi lililo kwenye hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo unaosababishwa na virusi.
Wanawake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mlipuko uliopita wa Ebola walikuwa theluthi mbili ya wagonjwa waliopatwa na ugonjwa huo kutokana na nafasi na mchango wa jadi i katika shughuli nyingiza kijamii.
Taarifa iliyotolewa wiki jana na UN Women imebainisha kuwa, wanawake wengi walipoteza maisha kwa ugonjwa wa Ebola miaka 50 iliyopita.
UN Women ilitahadharisha katika ripoti yake hiyo kwamba uhakika huo wa mambo ulishuhudiwa katika mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwaka 2018 hadi 2019 ambapo wanawake na wasichana walikuwa theluthi mbili ya kesi zilizoripotiwa.
Wahudumu wa Afya wameeleza kuwa mlipuko wa sasa wa Ebola pia unaweza kufuata mtindo huo wa mwaka 2018 hadi 2019.
Dakta Furaha Elisabeth Mkurugenzi wa Kliniki kwa jina la Karibuni Wamama Gynecology and Obstetrics katika mji wa Bunia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anasema kuwa " Anapougua mtu katika jamii; mwanamke ndiye hutoa huduma na kumsaidia mgonjwa. " Ni mwanamke ambaye humuogesha mgonjwa na kufanya shughuli zote ikiwa ni pamoja na kufua nguo za mgonjwa.
Dakta Furaha Elisabeth anasema: "Wauguzi (katika hospitali) kwa kawaida ni wanawake. Ikiwa muuguzi huyo wa kike ataambukizwa katika maeneo ya kazi ni rahisi sana kueneza maambukizi kwa watu wa karibu yake; na watu wa kwanza kuambukizwa watakuwa watoto wake. Ndiyo maana wanawake, mabinti wadogo, na watoto ndio watu walio katika hatari kubwa ya janga hili."