Waasi wa ADF wanaofungamana na ISIS waua watu 21 DRC
-
Waasi wa ADF
Idadi ya vifo kufuatia shambulio lililofanywa na waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF), kundi la waasi lenye misimamo mikali lililoanzia Uganda, imefikia 21 katika mji wa Mbau, ulioko mkoa wa Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Congo).
Ongezeko hilo la vifo limefuatia kupatikana kwa miili mingine kandokando ya mji baada ya shambulio hilo.
Mji wa Mbau ulikumbwa na shambulio la umwagaji damu usiku kati ya Jumanne na Jumatano. Kwa mujibu wa taarifa za awali zilizokusanywa na chombo cha habari cha ndani, Actualite, kutoka kwa manusura, wapiganaji wa ADF walifanya operesheni hiyo wakiwa wamegawanyika katika makundi matatu tofauti.
Waasi hao walilenga mitaa ya Matete, Kithoho na Mamuli, ambapo pia walichoma moto nyumba na pikipiki.
Louis Kisaki, kiongozi wa asasi ya kiraia ya Batangi-Mbau, akizungumza na wanahabari amesema: "Tungependa kuona jeshi likiwafuatilia washambuliaji hadi maficho yao ya mwisho, kwa sababu tutaangamizwa ikiwa hakuna hatua itakayochukuliwa."
Kwa mujibu wa chapisho hilo, waasi wa ADF wamewaua zaidi ya watu 40 katika mashambulizi yaliyotokea mjini Mbau na katika eneo pana la Beni katika siku tatu zilizopita. Raia kadhaa pia walitekwa nyara wakati wa mashambulizi hayo na bado wanashikiliwa. Waasi wa ADF wanadaiwa kufungamana na kundi la kigaidi la ISIS (Daesh)
Machafuko haya ya karibuni yanakuja wakati DR Congo ikiendelea kukabiliwa na kuzorota kwa hali ya usalama. Kundi la waasi la M23 bado linadhibiti sehemu za mashariki mwa nchi hiyo, jambo linalochangia kuendelea kwa mapigano ya silaha na kuzidisha changamoto za kibinadamu.
Hali ya usalama mashariki mwa DRC pia inazidi kuwa tata kutokana na kuenea ugonjwa hatari wa Ebola. Katika taarifa yake ya hivi karibuni, Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) viliripoti kuwa visa 1,077 vinavyoshukiwa vya Ebola pamoja na vifo 246 vinavyokadiriwa kuwa vya ugonjwa huo vimeandikishwa tangu tarehe 15 Mei, wakati DRC ilipotangaza rasmi mlipuko wake wa 17 wa Ebola.