WFP yalaani mashambulizi dhidi ya malori ya misaada kusini mwa Sudan
Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limetangaza kwamba malori yake mawili yalishambuliwa kutokea angani siku ya Jumapili nje ya eneo la Dilling la Jimbo la Kordofan Kusini, huko kusini mwa Sudan, wakati yalipokuwa njiani kupeleka chakula cha msaada kwa wakimbizi waliokwama kwenye eneo la Kadugli.
Kwa mujibu wa WFP, shambulio hilo liliharibu zaidi ya tani 50 za chakula. Kiwango hicho kilikuwa kinatosha kutoa msaada wa kuokoa maisha ya watu 5,800 kwa mwezi mzima. Katika taarifa yake, WFP imelaani vikali shambulio hilo na kusema kuwa, malori hayo yalikuwa na mabango na bendera za WFP zilizokuwa zinaonekana waziwazi.
Imesema, shambulio hilo ni uthibitisho wa hivi karibuni zaidi wa kuweko mazingira magumu ya uendeshaji yanayokabiliana nayo mashirika ya misaada ya kibinadamu nchini Sudan.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeziomba pande zote hasimu huko Sudan kuheshimu sheria ya kimataifa inayohusiana na masuala ya kibinadamu na wajibu wa kuwalinda raia, wafanyakazi wa masuala ya kibinadamu na mali. Huko Kadugli, WFP inasaidia karibu watu 58,000 wanaoishi ndani ya ukosefu mkubwa wa chakula.
Kundi jingine la kujitolea linalojiita "Wakili wa Dharura," nalo limelaani shambulio hilo likisema kwamba kushambulia misafara ya misaada ya kibinadamu ni sawa na kushambulia moja kwa moja raia ambao wako kwenye hali ngumu ya kimaisha.
Katika taarifa yake ya juzi Jumatano, kundi hilo lilionya kwamba mashambulizi kama hiyo yanazidisha tu migogoro ya kibinadamu katika kipindi hiki cha kupungua uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo na mvua chache.
Sudan imekwama kwenye mgogoro mkubwa wa mapigano ya silaha kati ya Jeshi la Sudan SAF na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF tangu katikati ya mwezi Aprili 2023. Maelfu ya watu wameshakufa hadi hivi sasa na mamilioni ya wengine wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.