Sep 02, 2016 04:14 UTC
  • Umoja wa Ulaya wazitaka pande hasimu Gabon kuvumiliana

Umoja wa Ulaya umeitaka serikali na wapinzani nchini Gabon kuvumiliana na kudumisha amani.

Federica Mogherini, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema katika tamko alilolitoa jana (Alkhamisi) kuwa, hali ya mambo nchini Gabon ni mbaya baada ya uchaguzi wa Rais na amezitaka pande hasimu zivumiliane.

Amesema, upinzani wowote ule inabidi uoneshwe kwa njia za amani ili kuipusha nchi hiyo kuingia kwenye machafuko.

Rais Ali Bongo Ondimba wa Gabon

 

Rais Bongo wa Gabon naye ametoa mwito wa kudumisha amani na umoja wa kitaifa nchini humo.

Kwa upande wake, Ban Ki moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewataka viongozi wa kisiasa na wafuasi wao nchini Gabon kujiepusha kuchukua hatua yoyote ya kuvuruga utulivu na kuitumbukiza nchi hiyo kwenye machafuko. 

Siku ya Jumanne, tume ya taifa ya uchaguzi ilimtangaza Ali Bongo Ondimba kuwa mshindi wa urais wa hivi karibuni, suala ambalo limepingwa vikali na wapinzani ambao walivamia Bunge la nchi hiyo na kulichoma moto.

Katika kujibu shambulizi hilo, vikosi vya kulinda usalama nchini Gabon vilishambulia makao makuu ya wapinzani, jambo ambalo limewafanya wapinzani hao waombe msaada kutoka kwa jamii ya kimataifa.

Tags