Vikosi vitiifu kwa Jenerali Haftar vyashambulia bandari za mafuta Libya
Vikosi vitiifu kwa Jenerali Khalifa Haftar kamanda wa kijeshi wa mashariki mwa Libya vimezishambulia bandari za mafuta nchini humo na kukabiliana na walinzi wa vituo hivyo.
Ali al Hassi Msemaji wa Petrol Facilities Guard (PFG) katika bandari hizo za mafuta ameeleza kuwa vikosi vitiifu kwa Jenerali Haftar vimezishambulia bandari za Zuweitina, Ras Lanuf na al Sidra mashariki mwa mji wa Sirte na kuushambulia pia mji wa karibu wa Ajdabiya na kusababisha mapigano. Mhandisi mmoja wa masuala ya bandari amethibitisha kujiri mashambulizi hayo ya vikosi vya Haftar na kueleza kuwa moja ya matanki ya kuhifadhia mafuta katika bandari ya a Sidra limechomwa moto kwenye makabiliano. Huku hayo yakiripotiwa Shirika la Habari la LANA lenye mfungamano na bunge la Libya linalotambuliwa kimataifa limemnukuu Kanali Ahmad Mesmari akisema leo kuwa, vikosi vitiifu kwa Jenerali Khalifa Haftar hivi sasa vinadhibiti bandari hizo tatu huko Sirte.