AI: Serikali ya Congo inawakandamiza wapinzani
Shirika la Msamahama Duniani (Amnesty International) limewatuhumu viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwa wanawakandamiza wapinzani.
Amnesty International imesema maafisa wa serikali ya Kinshasa wanatumia sera za kuwakandamiza na kuwanyanyasa wapinzani wa serikali ya Rais Joseph Kabila wanaomtaka kiongozi huyo ang'atuke madarakani baada ya kumalizika kipindi chake cha uongozi.
Shirika la Amnesty International limesisitiza kuwa, maafisa wa serikali ya Kinshasa wanatumia vyombo vya dola kwa ajili ya kuzuia maandamano na mikusanyiko ya wanaopinga suala la kubakia madarakani Rais Kabila baada ya kumalizika kipindi chake cha utawala.
Kipindi cha uongozi wa Rais Joseph Kabila kinamalizika tarehe 20 mwezi Disemba na kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kiongozi huyo haruhusiwi kugombea tena kiti cha rais.
Wakati huo huo wapinzani wa serikali ya Kinshasa wamesusia mazungumzo ya kitaifa yaliyoitishwa na Rais Kabila chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika. Kambi kuu ya upinzani inasema mazungumzo hayo ni mbinu inayotumiwa na Rais Kabila kwa shabaha ya kubakia madarakani baada ya kumalizika kipindi chake cha ungozi.