Waandamanaji wenye hasira washambulia viwanda vya makampuni ya kigeni nchini Ethiopia
Wananchi wenye hasira wamebomoa na kuharibu makumi ya viwanda vinavyomilikiwa na makampuni ya kigeni, mashamba ya maua pamoja na kuchoma moto magari kadhaa kulalamikia kile wanachoeleza uporaji ardhi zao unaofanywa na serikali nchini Ethiopia.
Machafuko yameikumba Ethiopia kufuatia vifo vya watu wasiopungu 55 mwishoni mwa wiki iliyopita wakati askari polisi walipotumia mabomu ya kutoa machozi na kufyatua risasi hewani kuwatawanya waandamanaji katika eneo la Oromiya karibu na mji mkuu Addis Ababa.
Kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu na wapinzani, kufuatia vifo hivyo idadi ya watu waliouawa katika machafuko yaliyoanza nchini Ethiopia tangu mwaka uliopita imepindukia 450 ingawa serikali inakanusha idadi hiyo.
Duru za habari zimeripoti kuwa majengo ya makampuni 11 yakiwemo ya viwanda vya nguo na utengezaji vifaa vya plastiki pamoja na mashamba ya maua yamebomolewa na kuharibiwa, na magari zaidi ya 60 yamechomwa moto. Miongoni mwa majengo yaliyobomolewa na mashamba yaliyoharibiwa ni ya makampuni ya Uholanzi na Uturuki.
Wananchi wa eneo la Oromiya wanaituhumu serikali ya Ethiopia inayolaumiwa pia kimataifa kwa kutumia mkono wa chuma kukandamiza wapinzani, kwamba imekuwa ikitwaa ardhi zao na kuwalipa kiwango kidogo mno cha fidia na kisha kuyauza, mara nyingi, kwa makampuni ya kigeni kwa bei juu mno.../