UN: Mustakabali wa kisiasa DRC umegubikwa na kiza
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17260-un_mustakabali_wa_kisiasa_drc_umegubikwa_na_kiza
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa hali ya kisiasa na kiusalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ipo katika hali nyeti hivi sasa na kwamba huenda machafuko yakashtadi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 12, 2016 04:26 UTC
  • UN: Mustakabali wa kisiasa DRC umegubikwa na kiza

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa hali ya kisiasa na kiusalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ipo katika hali nyeti hivi sasa na kwamba huenda machafuko yakashtadi.

Maman Sambo Sidikou, Mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo kuwa, pande hasimu za kisiasa DRC zimeshikilia misimamo mikali zikishinikiza ghasia na machafuko, badala ya kukumbatia mazungumzo ya amani.

Maandamano ya hivi karibuni ya wapinzani mjini Kinshasa, DRC

Ofisa huyo wa UN amesema binafsi hajaona mezani azimio lolote la kusuluhisha mgogoro huo wa kisiasa kwa njia ya amani na mazungumzo, jambo ambalo linaufanya mustakabali wa nchi hiyo usitabirike.

Kauli ya Umoja wa Mataifa imejiri muda mfupi baada ya kiongozi mmoja wa upinzani nchini humo kutiwa nguvuni kwa madai ya kuhusika na machafuko yaliyotokana na maandamano ya kupinga serikali yaliyofanyika mwezi uliopita, ambapo watu zaidi ya 50 waliuawa. Bruno Tshibala, Naibu Katibu Mkuu na msemaji wa chama kikuu cha upinzani nchini Kongo DR cha Muungano kwa ajili ya Demokrasia na Maendeleo ya Kijamii (UDPS)  alikamatwa katika uwanja wa ndege wa mji mkuu wa nchi hiyo Kinshasa wakati akijiandaa kupanda ndege kuelekea Brussels, Ubelgiji, hatua ambayo imeongeza wasiwasi wa kushuhudiwa maandamano zaidi ya upinzani endapo hatoachiwa huru.

Rais Joseph Kabila wa DRC

Kwa mujibu  wa katiba ya DRC, Rais Kabila ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2001, haruhusiwi kugombea tena kiti hicho baada ya kuhudumu kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano.