Nigeria yamkamata mjumbe wa Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17560-nigeria_yamkamata_mjumbe_wa_kiongozi_wa_harakati_ya_kiislamu
Vikosi vya usalama Nigeria vimemkamata mjumbe wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini humo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Oct 16, 2016 11:10 UTC
  • Sheikh Adamu Tsoho Ahmad
    Sheikh Adamu Tsoho Ahmad

Vikosi vya usalama Nigeria vimemkamata mjumbe wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini humo.

Duru zinadokeza kuwa, maafisa wa usalama leo Jumapili wamemkamata Shaikh Adamu Tsoho Ahmad, mwakilishi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambaye pia anashikiliwa korokoroni kwa karibu mwaka moja pasina kufunguliwa mashtaka. Sheikh Adamu Tsoho amekamatwa akiwa katika Kituo cha Kiislamu katika mji wa Jos katika Jimbo la Plateau kati mwa Nigeria.

Walioshuhudia tukio hilo wanasema, Jeshi la Nigeria limemkamata mwanazuoni huyo wa Kiislamu pasina kutoa sababu zozote na kumpeleka kusikojulikana.

Katika siku ya Ashura iiliyoadhimishwa Jumatano, jeshi la Nigria lilihujumu Husseiniya (ukumbi wa kidini) wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ambao walikuwa wakikumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS.

Mauaji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia

Katika hujuma hiyo, Waislamu 18 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Katika maeneo mengine ya Nigeria pia vikosi vya uslama viliwashambulia na kuwaua makumi ya Waislamu wa madheehbu ya Shia waliokuwa katika maombolezo ya Siku ya Ashura.

Wakuu wa jimbo la Kano kaskazini mwa Nigeria wametangaza kupiga marufuku Harakati ya Kiislamu nchini humo na kutoa amri ya kukamatwa msemaji wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo.

Ikumbukwe kuwa Disemba mwaka 2015, Jeshi la Nigeria liliwashambulia wafuasi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria katika mji wa Zaria jimboni Kaduna kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Jeshi hilo lilidai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inayoongozwa na Allamah Sheikh Ibrahim Zakzaky walikuwa na njama ya kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Nigeria, madai ambayo yamekanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo. Jeshi hilo katili liliizika miili ya waliouawa katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo. Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo huku Sheikh Zakzaky, ambaye hali yake ni mahututi, akiendelea kushikiliwa korokoroni pasina kufunguliwa mashtaka.