Daesh yafanya juhudi za kujizatiti kaskazini mwa Libya
Kundi la kigaidi la Daesh linafanya juhudi zake za mwisho za kulinda uwepo wake katika mji wa Sirte wa kaskazini mwa Libya.
Habari kutoka nchini Libya zinasema kuwa, kundi la Daesh limechimba mahandaki katika maeneo yote linayoyadhibiti huko Sirte kama njia ya kung'ang'ania maeneo ya mwisho iliyo nayo nchini Libya.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, baada ya kupita miezi sita ya opereseheni dhidi ya Daesh huko Libya, magaidi wa kundi hilo hivi sasa wamezingirwa katika eneo la ukubwa wa kilomita moja. Mji wa Sirte ulitekwa na magaidi wa ISIS mwaka mmoja uliopita na kuugeuza kuwa ngome yao kuu nchini Libya.
Iwapo mji wote wa Sirte utakombolewa, jambo hilo litakuwa ni pigo kubwa sana kwa genge la kigaidi la Daesh ambalo lina ngome pia katika nchi za Iraq na Syria.
Kundi la Daesh liliivamia Libya mwaka 2015 kutokana na kukosekana serikali moja yenye nguvu na kutokana na ugomvi mkubwa uliokuwepo baina ya makundi mbalimbali ya Libya.