Rais Museveni aiunga mkono Afrika Kusini kujiondoa ICC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18112-rais_museveni_aiunga_mkono_afrika_kusini_kujiondoa_icc
Rais Yoweri Museveni wa Uganda amepongeza hatua ya Afrika Kusini kuanzisha mchakato wa kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 25, 2016 04:20 UTC
  • Rais Museveni aiunga mkono Afrika Kusini kujiondoa ICC

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amepongeza hatua ya Afrika Kusini kuanzisha mchakato wa kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Akihutubia waandishi wa habari mjini Lusaka nchini Zambia hapo jana, Rais Museveni alisema uamuzi huo wa Afrika Kusini ni 'mzuri mno' na kwamba "ICC haina maana." Hata hivyo Rais Museveni alikwepa swali la wanahabari walipomuuliza iwapo Uganda itafuata mkondo huo wa Afrika Kusini na kujiondoa katika Mkataba wa Roma uliobuni mahakama hiyo iliyoko mjini Hague nchini Uholanzi.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC

Haya yanajiri siku chache baada ya serikali ya Sudan kuzitaka nchi za Afrika zijitoe ICC. Taarifa ya Ikulu ya Sudan ilisema kuwa, nchi za Afrika zinapaswa kujitoa kwenye mahakama hiyo kama ilivyofanya Afrika Kusini.

Hii ni katika hali ambayo, Michael Masutha, Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini hivi karibuni aliwaambia waandishi wa habari mjini Pretoria kuwa, nchi hiyo imewasilisha kimaandishi uamuzi wake wa kujitoa katika mahakama ya ICC kwa Ban Ki moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi

Aidha Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi amesaini mkataba wa kujiondoa nchi yake katika Makahama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Nchi kadhaa za Kiafrika zimetishia kujiondoa kwenye mahakama hiyo kutokana na hatua yake ya kuendelea kuwasakama viongozi wa nchi za bara hilo, huku ikifumbia macho jinai zinazofanywa na viongozi wa Magharibi.