Wahamiaji 2,200 wanusuriwa Mediterranea, miili 16 yapatikana
Wahamiaji karibu 2,200 wameokolewa katika Bahari ya Mediterranea katika oparesheni 21 za uokoaji huku miili 16 ikipatikana, Gadi ya Ulinzi wa Pwani ya Italia imesema.
Katika taarifa, gadi hiyo imesema oparesheni hiyo imehusisha meli kadhaa zikiwemo za uvuvi, mizigo na za mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu chini ya usimamizi wa Gadi ya Pwani ya Italia.
Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM zinaonesha kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2016 hadi sasa, karibu wahajiri laki moja na elfu 30 wameingia katika fukwe za Italia na wengi wao wametokea katika fukwe za Libya, huku zaidi ya 3,000 miongoni mwao wakiripotiwa kufa maji kabla ya kufika wanakokwenda, katika bahari ya Mediterranea. Aghalabu ya wahamiaji hao ni kutoka nchi za Kiafrika na pia Mashariki ya Kati.
Hivi karibuni, Rais Idris Deby wa Chad amesema ili kulipatia ufumbuzi jinamizi la wahajiri kumiminika barani Ulaya, sharti Umoja wa Ulaya uwahusishe viongozi wa Afrika katika mikakati yake ya kukomesha wimbi hilo la wahamiaji haramu.