Luteka ya pamoja ya kijeshi ya Russia na Misri yamalizika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18205-luteka_ya_pamoja_ya_kijeshi_ya_russia_na_misri_yamalizika
Televisheni ya al Ekhbariya ya nchini Syria imetangaza habari ya kumalizika mazoezi ya pamoja ya kijeshi baina ya Misri na Russia yaliyobeba kaulimbiu ya "Walinzi wa Urafiki 2016."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 26, 2016 11:47 UTC
  • Luteka ya pamoja ya kijeshi ya Russia na Misri yamalizika

Televisheni ya al Ekhbariya ya nchini Syria imetangaza habari ya kumalizika mazoezi ya pamoja ya kijeshi baina ya Misri na Russia yaliyobeba kaulimbiu ya "Walinzi wa Urafiki 2016."

Televisheni hiyo imenukuu taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Misri ikisema kuwa, zaidi ya wanajeshi 700 wameshiriki katika luteka hiyo ya kijeshi iliyoanza Jumapili ya tarehe 16 Oktoba katika eneo ka jangwani la kaskazini magharibi mwa Cairo, mji mkuu wa Misri, na ndani yake kumetumika mbinu mbalimbali za kijeshi katika nyuga tofauti.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maeneo makuu yaliyozingatiwa katika maneva hayo ni kuongoza vita vya mijini, kupambana na ugaidi na kukomboa mateka na watu wanaoshikiliwa na maadui kwa ushirikiano wa pamoja baina ya jeshi la anga na brigedi nyingine za kijeshi.

Rasi ya Sinai ya kaskazini mwa Misri imekuwa uwanja wa mapigano kwa miaka kadhaa sasa

 

Wakati huo huo vyombo vya habari vya Russia vimetangaza kuwa, Moscow imeanzisha mazungumzo na Misri kwa ajili ya kuanzisha kambi ya jeshi la anga katika ardhi ya Misri. Hata hivyo, vyombo vya habari vya Misri vimemnukuu msemaji wa rais wa nchi hiyo akikanusha habari hiyo.