Wahajiri 239 wafariki dunia pwani ya Libya wakielekea Ulaya
Umoja wa Mataifa umesema wahajiri 239 wali0kuwa wakielekea barani Ulaya wamepoteza maisha baada ya boti zao kuzama katika pwani ya Libya.
Carlotta Sami, msemaji wa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amethibitisha habari hizo na kusema kuwa, miili ya wahajiri hao imepatikana katika boti mbili pwani ya Libya na kwamba manusura wamepelekwa katika kisiwa cha Lampedusa, pwani ya Italia.
Mapema mwezi huu, gadi ya ulinzi wa pwani ya Italia ilisema wahajiri wapatao 5,600 wamenusurika kifo katika pwani ya Libya kwenye bahari ya Mediterranean wakielekea barani Ulaya; idadi inayotajwa kuwa kubwa zaidi ya wahajiri kuokolewa katika siku moja.
Hivi karibuni, Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR lilisema kuwa, aghalabu ya wahajiri wanaopoteza maisha katika ajali hizo za boti ni raia wa nchi za Kiafrika kama Somalia, Sudan, Ethiopia na Misri.
Kwa mujibu wa Leonard Doyle, Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM, wahajiri karibu laki mbili wameingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranean katika mwaka huu pekee huku wengine zaidi ya 4,200 wakifariki dunia kwa kuzama baharini. Mwaka jana 2015, wahajiri 3,770 wanaaminika kufa maji baada ya boti zao kutohimili mawimbi ya bahari walipokuwa wakielekea barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranean.