Mgomo na maandamano ya wanafunzi nchini Uganda vyasimamisha masomo
Maandamano na mgomo wa wanafunzi nchini Uganda vimesababisha shughuli za masomo kusimama nchini humo.
Jumanne ya leo wanafunzi wa vyuo vikuu vya miji ya Kampala na Mbarara wamefanya maandamano makubwa mbele ya ofisi za serikali kulalamikia sera mbovu za elimu na utamaduni nchini. Kufuatia hali hiyo polisi maalumu waliimarisha doria nje ya vyuo vikuu vya miji hiyo ambapo sanjari na kuwatawanya wanafunzi hao, imewatia mbaroni kadhaa miongoni mwao.
Habari zaidi zinaeleza kuwa jumuiya kadhaa za wanafunzi zimetoa ripoti kwa nyakati tofauti na kuitaka serikali ya nchi hiyo itilie mkazo mapendekezo na matakwa ya kisheria ya wanafunzi na walimu wao ili kuboresha elimu. Wawakilishi wa jumuiya hizo za wanafunzi nchini Uganda wamesema kuwa umefika wakati kwa serikali ya Kampala kuangalia upya siasa za elimu kwa faida ya watu wa matabaka yote katika jamii.
Kadhalika jumuiya hizo za wanafunzi zimesisitiza kuendeleza maandamano hayo siku chache zijazo hadi yatakapofikiwa malengo yao yote. Hayo yanajiri katika hali ambayo hivi karibuni Mahakama Kuu ya Uganda ilitoa hukumu ya kufungwa shule 63 za binafsi za Kimarekani zinazofanya kazi nchini humo kutokana na kutokuwa na viwango vinavyotakiwa.
