Mpinzani ateluwa kuwa Waziri Mkuu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amemteua mbunge wa kambi ya upinzani kuwa waziri mkuu baada ya mapatano baina ya serikali na baahdi ya makundi ya upinzani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyorushwa hewani kupitia televisheni ya kitaifa Alhamisi, Kabila amemteua Samy Badibanga kuwa waziri mkuu baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Agustin Matata kujiuzulu kama sehemu ya mapatano baina ya serikali na upinzani.
Kwa mujibu wa mapatano hayo, serikali itagawana madaraka na baadhi ya vyama vya upinzani katika kipindi cha mpito kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Hatahivyo mapatano hayo yalisusiwa na vyama vikuu vya upinzani.
Badibanga alishiriki katika mazungumzo na serikali ya Kabila mwezi Oktoba ambapo sasa rais huyo atasalia madarakani baada ya muhula wake kumalizika mwezi ujao. Kwa mujibu wa mapatano hayo, kwa uchache Kabila atasalia madarakani hadi mwishoni mwa mwaka 2017.
Mazungumzo hayo baina ya serikali na baadhi ya wapinzani DRC yalianza baada ya machafuko ya kisiasa ya mwezi Septemba ambapo watu zaidi ya 53 waliuawa. Baadhi ya wapinzani, wakiongozwa na mwanasiasa mkongowe, Etienne Tshisekedi wa UDPS, wanapinga mapatano ya sasa na kusisitiza kuwa Kabila lazima aondoke madarakani mwaka huu.