Libya; njia kuu ya wahajiri wengi
Shirika la Kimataifa la Wahajiri limetangaza kuwa Libya ni njia kuu inayotumiwa na wahajiri wengi licha ya nchi hiyo kukabiliwa na mgogoro wa ndani.
Shirika la Kimataifa la Wahajiri limesema katika ripoti yake ya wiki hii kwa mujibu wa uchunguzi mmoja wa maoni uliofanywa kwamba, asilimia 56 ya wahajiri wote ambao wako nchini Libya hawana lengo la kuelekea Ulaya bali wanapendelea kubakia katika nchi hiyo ya Kiafrika. Shirika hilo limeongeza kuwa asilimia 81 hadi 83 ya wahajiri kutoka Misri, Chad na Sudan wanapendelea kubaki Libya huku asilimia 43 wa wahajiri wengine wakitaka kuelekea barani Ulaya.
Uchunguzi huo wa maoni umefanyika baada ya kuhojiwa wahajiri 1946 katika maeneo 9 ya Libya. Pamoja na hayo yote, Shirika la Kimataifa la Wahajiri limetangaza katika ripoti yake mpya kuhusu majeruhi wa baharini huko Libya kuwa, wahamiaji 440 waliokolewa katika maji ya nchi hiyo kati ya tarehe 4 hadi 18 za mwezi huu wa Novemba.