Wasiwasi wa kuzidi kuongezeka mgogoro wa kibinadamu nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20587-wasiwasi_wa_kuzidi_kuongezeka_mgogoro_wa_kibinadamu_nchini_libya
Kuzidi kuwa mkubwa mgogoro wa kisiasa nchini Libya kumemfanya mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa aelezee masikitiko yake makubwa kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu na kiusalama ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 02, 2016 02:56 UTC
  • Wasiwasi wa kuzidi kuongezeka mgogoro wa kibinadamu nchini Libya

Kuzidi kuwa mkubwa mgogoro wa kisiasa nchini Libya kumemfanya mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa aelezee masikitiko yake makubwa kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu na kiusalama ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Martin Kobler, mwakilishi wa kudumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya aidha ameelezea kuchukizwa kwake na hatua zilizochukuliwa za kudhibiti mwenendo wa wahamiaji nchini Libya na kuongeza kuwa, magendo ya wanadamu yataendelea nchini Libya maadamu hakuna serikali yenye nguvu ya kudhibiti mambo yote nchini humo.

Matamshi ya Martin Kobler yametolewa katika hali ambayo kamati ya ngazi za juu ya Umoja wa Afrika iliyoundwa kwa kazi maalumu ya kushughulikia kadhia ya Libya ilisema mwezi uliopita kuwa, mchakato wa kisaisa nchini Libya umekwama kikamilifu na kwamba wanaodhuriwa zaidi na hali hiyo ni wananchi wa kawaida.

Martin Kobler, mwakilishi wa kudumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya

Libya imeshindwa kuwa na utulivu tangu alipopinduliwa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011. Nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika inakabiliwa na migogoro mingi na imegeuka kuwa eneo la kujifichia magenge ya kigaidi, likiwemo kundi la wakufurishaji la Daesh (ISIS). Takwimu zinaonesha kuwa, kuna zaidi ya makundi 1,700 ya wanamgambo katika maeneo tofauti ya Libya hivi sasa

Martin Kobler amesema, mgogoro wa kiusalama na kibinadamu nchini Libya unatia wasiwasi na kwamba katika kipindi chake chote cha kuhudumu kama mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa hataweza kutatua mgogoro huo bali jukumu la kutatua jambo hilo litakuwa ni la vizazi vijavyo.

Mgogoro wa kisiasa nchini Libya umesababisha matatizo makubwa ya kibinadamu na madhara yake yanawaelemea wananchi wa kawaida wanaoishi kwenye umaskini mkubwa hivi sasa na wengi wao wanahitajia misaada ya chakula na madawa na hakuna uwezekano wa kuwafikishia misaada hiyo kutokana na hali mbaya ya kiusalama inayotawala Libya hivi sasa.

Mapigano yanaendelea nchini Libya tangu wakati wa kampeni za kumpindua Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011

Hii ni katika hali ambayo migogoro ya kisiasa haioneshi dalili yoyote ya kupungua nchini Libya na hali hiyo imepelekea magenge mbalimbali ya kigaidi kujiingiza na kujiimarisha nchini humo ijapokuwa katika miezi ya hivi karibuni serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya imefanikiwa kulifurusha genge la kigaidi la Daesh katika maeneo mengi ya nchi hiyo, lakini hadi hivi sasa bado genge hilo lina watu wake ndani ya Libya na hiyo ni hatari kwa usalama wa nchi hiyo.

Kundi la Daesh liliigeuza Libya kuwa kituo chake kikuu cha kuwapa mafunzo magaidi wanaofanya mashambulizi katika nchi jirani na Libya kama vile Tunisia na Misri. Vile vile kuweko magenge ya magendo ya binadamu ndani ya Libya, ni mgogoro mwingine unaoikabili Libya hivi sasa.

Cha kuzingatia hapa ni kuwa, Libya ndilo lango pekee la wahajiri kutoka nchi mbalimbali za Afrika kuelekea barani Ulaya. Libya hivi sasa ina hali mbaya ya kiuchumi na kiusalama na hakuna serikali kuu yenye nguvu, suala hilo limetoa mwanya kwa magenge ya magendo ya binadamu kufanya kazi zao kwa upana nchini humo. Wengi wa wahajiri hao huangukia mikononi mwa magenge ya wahalifu ambayo huwateka nyaraka kwa lengo la kupata fedha za kikomboleo na wengi wa wahajiri huteswa na kushikiliwa kwenye korokoro za kuogofya na makundi hayo. 

Kuna uharibifu mkubwa wa miundombinu kutokana na mapigano ya muda mrefu nchini Libya.

 

Ijapokuwa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya kulileta matumaini ya kubadilika hali ya mambo nchini humo, lakini kuna makundi mengi ndani ya Libya hadi leo hii yamekataa kuitambua serikali hiyo na jambo hilo limeifanya ishindwe kudhibiti hali ya mambo. Muhtasari wa maneno hayo ni kwamba, hivi sasa Libya imekwama kisiasa na iko katika hali mbaya ya kibinadamu kiasi kwamba hata mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa amelazimika kukiri kwamba, hana uwezo wa kutatua mgogoro huo na hakuna uwezekano wa kutengenea hali ya Libya katika kipindi chote cha kuhudumu kwake kama mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini humo.