Yahyah Jammeh ashindwa vibaya katika uchaguzi wa rais Gambia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20608-yahyah_jammeh_ashindwa_vibaya_katika_uchaguzi_wa_rais_gambia
Rais Yahyah Jammeh wa Gambia amekiri kushindwa katika uchaguzi wa rais nchini humo na kwa msingi huo kuhitimisha utawala wake wa miaka 22 katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Dec 02, 2016 12:14 UTC
  • Yahyah Jammeh  ashindwa vibaya katika uchaguzi wa rais Gambia

Rais Yahyah Jammeh wa Gambia amekiri kushindwa katika uchaguzi wa rais nchini humo na kwa msingi huo kuhitimisha utawala wake wa miaka 22 katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Kwa mujibu wa taarifa ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Gambia Alieu Momarr Njai, katika uchaguzi uliofanyika Alhamisi, rais wa sasa wa nchi hiyo ameshindwa na mpinzani wake Adama Barrow aliyepata asilimia  45.5 ya kura huku Jammeh akipata asilimia 36.7.

Jammeh amekubali kushindwa hata kabla ya kura kumalizika kuhesabiwa jambo ambalo limewashangaza wengi kwani aliwahi kusema ataitawala nchi hiyo kwa 'miaka billioni'. Mapema wiki hii Jamme alinukuliwa akisema, 'urais na nguvu zote ziko mikononi mwa Allah na ni Allah anayeweza kuuchukua urais."

Masanduku ya kupigia kura Gambia

Rais mteule Barrow ameweza kwa mara ya kwanza kuwaleta pamoja wapinzani wote Gambia na ameahidi kufufua uchumi wa nchi hiyo ambao kuporomoka kwake kumesababisha maelfu ya Wagambia kukimbilia Ulaya kutafuta maisha bora.

Uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa wa kwanza mgumu kwa Jammeh tokea anyakue madaraka nchini humo mwaka 1994 kupitia mapinduzi ya kijeshi. Katika muda wote huo amekuwa akiitisha chaguzi ambazo alishinda kwa kuibua hitilafu za kikabila miongoni mwa wapinzani.