Mahakama ya Nigeria yaamuru Sheikh Zakzaky aachiliwe huru
Mahakama nchini Nigeria imeiamuru serikali kumuachilia huru Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini humo Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Katika hukumu iliyotolewa leo Ijumaa, Jaji Gabriel Kolawole wa Kitengo cha Abuja cha Mahakama Kuu ya Nigeria ameiamuru serikali kumuachilia huru Sheikh Zakzaky na mke wake katika kipindi cha siku 45.
Jaji huyo ameonya kuwa, iwapo Sheikh Zakzaky atapoteza maisha akiwa gerezani, jambo hilo linaweza kuibua ghasia na kupelekea idadi kubwa ya watu kupoteza maisha.
Sheikh Ibrahim Zakzaky amekuwa akishikiliwa na vyombo vya usalama vya Nigeria kwa karibu mwaka mmoja sasa bila ya kufunguliwa mashtaka hatua ambayo imekuwa ikilalamikiwa na taasisi za kutetea haki za binadamu.
Tangu mwanazuoni huyo atiwe mbaroni, takwa kuu la jamii ya Waislamu nchini Nigeria ni kuachiliwa huru mwanaharakati huyo wa Kiislamu na kuheshimiwa haki zake za kibinadamu. Aidha jamii ya Waislamu nchini Nigeria inaitaka serikali ya nchi hiyo iheshimu haki za Waislamu wa nchi hiyo.
Disemba 13 mwaka jana jeshi la Nigeria lilifanya hujuma dhidi ya Husseiniyah ya Baqiyatullah na makazi ya Sheikh Zakzaky mjini Zaria. Waislamu wapatao elfu moja waliuawa kwa umati na jeshi hilo likamtia mbaroni Sheikh Zakzaky pamoja na mkewe.
Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky imezorota huku maafisa wa usalama wakizuia mwanazuoni huyo kupatiwa matibabu.