Makumi ya raia waokolewa kutoka mikononi mwa magaidi nchini Libya
Habari kutoka nchini Libya zinasema kuwa, jeshi la serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo limefanikiwa kuwaokoa makumi ya raia waliokuwa wametekwa nyara na genge la kigaidi na la wakufurishaji la Daesh mjini Sirte.
Wanajeshi wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya walisema jana kuwa, mji wa Sirte umekaribia kusafishwa kikamilifu na wamefanikiwa kuwakomboa karibu raia 41 kutoka mikononi mwa genge la kitakfiri la Daesh (ISIS).
Vyombo vya habari vimeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wanajeshi wa serikali ya Libya wameongeza nguvu zao katika eneo la "al Jiza al Bahriyyah" ambalo linahesabiwa kuwa ndicho kituo cha mwisho cha genge la Daesh mjini Sirte.
Genge hilo limefanya jinai kubwa dhidi ya wanawake na watoto wadogo na limekuwa likiwatumia kama ngao ya kibinadamu ya kujikinga na mashambulizi ya askari wa serikali.
Libya imeshindwa kuwa na utulivu tangu alipopinduliwa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011. Nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika inakabiliwa na migogoro mingi na imegeuka kuwa eneo la kujifichia magenge ya kigaidi, likiwemo kundi la wakufurishaji la Daesh (ISIS). Takwimu zinaonesha kuwa, kuna zaidi ya makundi 1,700 ya wanamgambo katika maeneo tofauti ya Libya hivi sasa.
Mgogoro wa kisiasa nchini Libya umesababisha matatizo makubwa ya kibinadamu na madhara yake yanawaelemea wananchi wa kawaida wanaoishi kwenye umaskini mkubwa sasa hivi na wengi wao wanahitajia misaada ya chakula na madawa na hakuna uwezekano wa kuwafikishia misaada hiyo kutokana na hali mbaya ya kiusalama inayotawala Libya hivi sasa.